WATANO WAFA AJALI YA HELIKOPTA MLIMA KILIMANJARO

 WATANO WAFARIKI KATIKA AJALI YA HELIKOPTA MLIMA KILIMANJARO

Na Arushadigital -KILIMANJARO





Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limethibitisha vifo vya watu watano kufuatia ajali ya helikopta iliyokuwa ikihudumia watalii katika Mlima Kilimanjaro, tukio lililotokea jioni ya Desemba 24, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), helikopta hiyo ilianguka katika eneo la barafu juu ya Mlima Kilimanjaro majira ya saa kumi na moja na nusu jioni, ikiwa imebeba watu watano.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa helikopta hiyo inayomilikiwa na Kampuni ya KilimediAIR, aina ya Airbus AS350 B3, ilikuwa imewabeba watalii wawili raia wa Jamhuri ya Czech, pamoja na raia wawili wa Tanzania ambao ni muongoza watalii mmoja na daktari mmoja. Mtu wa tano alikuwa rubani wa helikopta hiyo, raia wa Zimbabwe. Wote walipoteza maisha katika ajali hiyo.

Chanzo cha ajali hiyo bado hakijabainika rasmi. TANAPA imesema kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Mamlaka ya Usalama wa Anga, uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini sababu za kuanguka kwa helikopta hiyo.

Tukio hilo limeleta majonzi makubwa kwa familia za marehemu, sekta ya utalii pamoja na wadau wa uhifadhi, huku mamlaka husika zikiahidi kutoa taarifa zaidi pindi uchunguzi utakapokamilika.



Post a Comment

0 Comments