TEMDO Katika Mkakati Mpya wa Taifa, Katambi Aitaka Iwe Injini ya Viwanda
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Akizungumza leo desemba 23,2025 wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo jijini Arusha, Katambi amesema TEMDO ni mhimili muhimu katika utekelezaji wa agenda ya taifa ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa ina jukumu la kubuni, kuzalisha na kusambaza mitambo inayokidhi mahitaji ya wananchi, taasisi za umma na sekta binafsi.
Ameeleza kuwa uzalishaji wa mitambo ya ndani utaongeza thamani ya rasilimali za ndani, kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuimarisha ajira kwa Watanzania.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alipotembelea karakana za uzalishaji mitambo, amezitaka taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa utoaji wa ajira, mafunzo kwa vitendo na kukuza ubunifu kwa vijana, ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi na sekta binafsi ili vijana wengi zaidi washiriki kikamilifu katika mapinduzi ya viwanda, hasa katika nyanja za uhandisi, teknolojia na ubunifu wa mitambo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, Profesa Frederick Kahimba, amesema taasisi hiyo inaendelea kuimarisha uwezo wake wa kitaalamu na kiteknolojia kwa kuwekeza katika tafiti, ubunifu, rasilimali watu na miundombinu ya kisasa, ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mitambo inayozalishwa nchini.
Prof. Kahimba ameongeza kuwa TEMDO inaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za elimu ya juu, viwanda na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kuhakikisha teknolojia zinazobuniwa zinakuwa na tija ya moja kwa moja kwa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi.
Naye mmoja wa wanufaika wa huduma za TEMDO, Bi. Beatrice Msafiri, amesema kupitia ushauri wa kitaalamu, mafunzo na mitambo iliyozalishwa na TEMDO, ameweza kupanua shughuli zake za kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kuajiri vijana wengine, hatua iliyomsaidia kuboresha kipato chake na kuchangia maendeleo ya jamii.
Kwa sasa, TEMDO imejikita katika uzalishaji wa mitambo ya kilimo, vipuri mbalimbali, vifaa tiba pamoja na teknolojia na mashine zinazosaidia Serikali na sekta binafsi kupunguza gharama kubwa za uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, huku ikiimarisha dhana ya “Buni Tanzania, Tumia Tanzania” na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, shindani na endelevu.
Mwisho.



0 Comments