Breaking🔥

ASKARI WATATU WA HIFADHI NGORONGORO WALIOUA RAIA WALIOPOTEA WATIWA MBARONI

Askari Ngorongoro watatu mbaroni kwa mauaji ya mtu mmoja waliopotea njia

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

JESHI LA POLISI Mkoa wa Arusha limeanza uchunguzi wa tukio la kifo cha fundi gereji mmoja na kujeruhiwa kwa mwenzake, baada ya watu hao watatu wanaodaiwa kuingia ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kinyume na utaratibu, kukamatwa na askari wa uhifadhi.

Tukio hilo linadaiwa kutokea baada ya watu hao, ambao wote ni wakazi wa Jiji la Arusha, kukamatwa Agosti 12, 2026, huku mmoja wao akifariki dunia, mwingine akijeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Lutheran Karatu, wakati mtu wa tatu akifanikiwa kurejea jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema Jeshi hilo lilipokea taarifa kuhusu watu wawili wa kiume waliofikishwa katika Hospitali ya Lutheran, mmoja akiwa tayari amefariki na mwingine akiwa hai na akiendelea kupatiwa matibabu.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, askari wa Polisi walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa awali, ikiwamo kubaini chanzo cha kifo na iwapo kilisababishwa na mtu, pamoja na kubaini waliohusika na mazingira ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa SACP Masejo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa aliyefikishwa hospitalini akiwa amefariki dunia alitambulika kwa jina la Sefu Mussa (25), fundi gereji na mkazi wa Matejo, Jijini Arusha.

Mtu mwingine aliyekuwa hai na anaendelea kupatiwa matibabu ametajwa kuwa ni Salimu Haji, maarufu Chambega, ambaye pia ni fundi gereji na mkazi wa Makao Mapya, Jijini Arusha.

Kamanda Masejo alisema uchunguzi zaidi umebaini kuwa wawili hao walikuwa pamoja na mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Abdallah Nuru, maarufu Ngandana, fundi gereji na mkazi wa Matejoo, Arusha.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali, Abdallah ndiye aliyekuwa akiendesha pikipiki iliyowabeba watu hao watatu.

SACP Masejo alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa watu hao walikamatwa na askari wa uhifadhi Ngorongoro majira ya saa nne asubuhi, Agosti 12, baada ya kupotea na kuingia katika eneo la hifadhi bila kufuata utaratibu unaotakiwa.

Aidha, inadaiwa walikuwa na pikipiki ambazo haziruhusiwi kuingia katika eneo hilo la hifadhi.

Baada ya kukamatwa na kuhojiwa, watu hao walidai kuwa walikuwa wametokea Jijini Arusha wakielekea Babati kuhudhuria msiba, lakini walipotea njia na kujikuta wameingia ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuchunguza maelezo hayo ili kubaini kwa kina kilichotokea kuanzia wakati wa kukamatwa kwao na askari wa uhifadhi hadi mmoja wao kufariki dunia, mwingine kujeruhiwa na wa tatu kurejea Jijini Arusha.

Katika hatua nyingine, Kamanda Masejo amesema askari watatu waliokuwa zamu katika eneo ambalo watu hao wanadaiwa kukamatwa wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi.

Alisema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa Jeshi hilo kupata ukweli wa tukio hilo na kubaini iwapo kuna ukiukwaji wowote wa sheria au taratibu uliohusika katika mazingira yaliyopelekea kifo cha Sefu Mussa na majeraha aliyopata Salimu Haji.

Kamanda Masejo alisema Polisi tayari imeanza kupata maelezo kutoka kwa baadhi ya watu wanaoweza kusaidia kutoa mwanga kuhusu tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea.

Alisisitiza kuwa taarifa zilizopo kwa sasa ni za awali na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli kamili wa tukio hilo kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.

Uchunguzi huo unatarajiwa pia kubaini kwa nini watu hao waliingia katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, mazingira ya kukamatwa kwao, pamoja na matukio yaliyofuata hadi mmoja wao kupoteza maisha na mwingine kuishia hospitalini.

Ends

NB.Picha kwa hisani ya mitamdao  !

Post a Comment

Previous Post Next Post