POLISI MWANAMKE APANDISHWA CHEO KWA KUKATAA RUSHWA YA DOLA 50,000(124 ML)

Polisi Mwanamke Zambia Apandishwa Cheo kwa Kukataa Hongo ya Dola 50,000

By Arushadigtal-ZAMBIA

LUSAKA, Zambia — Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zambia (ACC) imetangaza kumpandisha cheo polisi mwanamke aliyedhihirisha uadilifu wa hali ya juu baada ya kukataa hongo ya Dola za Kimarekani 50,000 (sawa na Shilingi milioni 124) kutoka kwa mshukiwa mkubwa wa ulanguzi wa fedha haramu katika Uwanja Mkuu wa Ndege wa Kimataifa wa Lusaka.

Polisi huyo, Sajenti wa Upelelezi Ruth Nyambe, aliyekuwa akihudumu katika Kitengo cha Usalama wa Viwanja vya Ndege, alikataa kupokea hongo hiyo kutoka kwa mshukiwa ambaye, wakati wa uchunguzi, alikutwa na fedha taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 2.3 (takribani Shilingi bilioni 5.7) pamoja na vipande saba vya dhahabu, vinavyodhaniwa kuwa ni sehemu ya mtandao wa uhalifu wa kifedha wa kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya ACC, mshukiwa huyo—ambaye jina lake halikutajwa kwa sababu za kisheria—alijaribu kumpa Nyambe hongo ya awali ya Dola 5,000 ili aruhusiwe kuendelea na safari yake. Hata hivyo, baada ya Nyambe kukataa, mshukiwa huyo aliongeza ofa hiyo hadi kufikia Dola 50,000, jaribio ambalo nalo liligonga mwamba kutokana na msimamo thabiti wa uadilifu wa polisi huyo.

Kutokana na kitendo hicho cha kuzingatia maadili ya kazi na sheria, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Zambia, Graphel Musamba, siku ya Jumatano alimpandisha cheo Ruth Nyambe kutoka Sajenti hadi Inspekta wa Polisi, hatua iliyopokelewa kwa pongezi kubwa ndani na nje ya jeshi hilo.

Jeshi la Polisi Zambia limesema kuwa kupandishwa cheo kwa Nyambe ni ishara ya kutambua na kuthamini uadilifu, uzalendo na utendaji kazi wa hali ya juu, sambamba na kuhimiza maafisa wengine kuzingatia maadili ya kazi na kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa.

Hatua hiyo pia imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali ya Zambia wa kuimarisha vita dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha, hususan katika maeneo nyeti kama viwanja vya ndege vinavyotumika kama njia za kusafirisha fedha haramu na mali zenye asili isiyojulikana.

Ends .

Post a Comment

0 Comments