By Arushadigital
Watuhumiwa watatu wa utekaji na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Shyrose Mahande, wamefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa risasi wakati wakijaribu kutoroka polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea baada ya jeshi hilo kuanza ufuatiliaji kufuatia taarifa za mauaji ya Shyrose zilizoripotiwa Septemba 14, mwaka huu.
Amesema mnamo Septemba 24 na 25, polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu waliotajwa kwa majina ya Marwa Nyahega, Edward Kayuni na Websta Mwantebele, lakini walifariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa risasi walipojaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.
Kamanda Kuzaga ameongeza kuwa, licha ya vifo hivyo, jeshi la polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine, akiwemo mganga wa kienyeji anayedaiwa kupelekewa sehemu ya viungo vya marehemu Shyrose Mahande aliyenyongwa .
0 Comments