By Arushadigital
Mnamo Septemba 14, 2025 liliripotiwa tukio la kutekwa nyara kwa Shyrose Michael Mabula [21] aliyekuwa mwanachuo mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ndaki ya Mbeya Kitivo cha Sheria na watu wasiofahamika, ambapo Septemba 16, 2025 saa 5:00 usiku huko Mtaa wa Morovian uliopo Kata ya Isyesye Jijini Mbeya mwili wa mwanachuo huyo ulikutwa ukiwa umechomwa moto.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza ufuatiliaji ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika katika tukio hilo na Septemba 24, 2025 saa 4:00 asubuhi alikamatwa Marwa Nyahega John [25] mkazi wa Uzunguni “A” Mbeya ambaye katika mahojiano alikiri kuwa yeye pamoja na wenzake wawili ambao ni Edward Christopher Kayuni na Websta William Mwantebele kwa pamoja walikula njama na kumteka nyara Shyrose Michael Mabula [ambaye kwa sasa ni marehemu] kwa lengo la kujipatia fedha nyingi kutoka kwa baba yake mzazi aitwaye Dkt Mabula Michael.
Baada ya kumteka walianza kupiga simu kwa familia yake kwa lengo la kujipatia fedha na iliposhindikana kupata fedha hizo kwa kuhofia kwamba watakamatwa walipanga kumuua binti huyo ili kupoteza ushahidi. Awali walimnywesha sumu ambayo ni dawa ya kuulia magugu mashambani aina ya “Round Up” iliposhindikana kuondoa uhai wake waliamua kumnyonga kwa kamba hadi kufa kisha kuuchoma moto mwili wake.
Baada ya kupata taarifa hiyo ufuatiliaji uliendelea na Septemba 25, 2025 alikamatwa mtuhumiwa Websta William Mwantebele [27] Mlinzi ambaye alikiri kushiriki kufanya tukio la utekaji na mauaji ya binti huyo na kueleza kuwa tukio hilo walifanya kwa kushirikiana na wenzake ambao ni Marwa Nyahega John na Edward Christopher Kayuni. Aidha alieleza kuwa anaweza kwenda kuwaonyesha Askari watuhumiwa wenzake kwani wamepanga kwenda mafichoni kwenye machimbo yaliyopo Wilayani Chunya.
Septemba 27, 2025 aliwapeleka Askari Polisi katika Kijiji cha Chalangwa eneo walilokuwa wamepanga kukutana. Askari Polisi waliweka mtego kwa ajili ya kumkamata mtu ambaye Websta William Mwantebele [Mtuhumiwa] atawaonyesha. Baada ya muda alifika mtu mmoja na mtuhumiwa huyo akawaeleza Askari kuwa huyo anayekuja ndiye Edward Christopher Kayuni waliyeshirikiana naye kumuua binti huyo.
Kamanda Kuzaga amesema msako unaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine akiwemo mganga wa jadi aliyepokea baadhi ya vitu vya marehemu. Aidha, ametoa onyo kali kwa vijana na wananchi kuachana na tamaa ya mali kupitia vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa uhalifu haulipi.
@polisi.tanzania
0 Comments