VIFAA VYA KISASA VYA TIBA VYAKABIDHIWA KAGERA ILI KUREJESHA HALI BAADA YA MLIPUKO WA MARBURG !

 VIFAA VYA KISASA VYA TIBA VYAKABIDHIWA  KAGERA ILI KUREJESHA HALI BAADA YA MLIPUKO WA MARBURG 

Na Lydia Lugakila 

Kagera


Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya , wamekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 112 kwa serikali ya Mkoa wa Kagera. 


Vifaa hivyo vitatumika katika halmashauri za Biharamulo na Muleba katika juhudi za kurejesha hali baada ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg.


Mkurugenzi Mkazi wa WHO, Dr. Galberth Fadjo, amesisitiza umuhimu wa kuwa na hatua za haraka katika kukabiliana na magonjwa hatari, huku akitoa wito kwa mamlaka kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi.


Aidha Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda vya kisasa vya kulaza wagonjwa, Mashine za kusafisha mashuka, stendi za kuwekea dawa

 ndoo za kuhifadhi maji na kufanyia usafi pamoja na vifaa vya kufanya uchunguzi wa kina.


Dr. Fadjo amepongeza serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za kukabiliana na milipuko ya magonjwa, akitolea mfano wa namna nchi hiyo ilivyoweza kudhibiti mlipuko wa Marburg wilayani Bukoba mwaka 2023.



Naye Dr. Erasto Sylvanus kutoka wizara ya Afya amesema kujenga ushirikiano na wadau ni muhimu katika kukabiliana na magonjwa hatari.


 Amepongeza kuwa Vifaa vilivyotolewa vitaimarisha ujuzi na utendaji wa wataalamu wa afya katika Mkoa wa Kagera.


Dr. Sylvanus ametoa wito kwa halmashauri za Mkoa wa Kagera kutenga bajeti ya ndani kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa

 Steven Ndaki amesisitiza juu ya umuhimu wa kutunza vifaa vilivyotolewa na kuongeza mafunzo kwa wataalamu, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa.


Mkoa wa Kagera umejipanga kuendelea kukabiliana na milipuko ya magonjwa, huku ukizingatia mipaka yake na nchi nyingine ambazo zinaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.


Ikumbukwe kuwa vifaa hivyo vitasaidia katika kuongeza uwezo wa serikali kugharamia matukio ya dharura ya afya.






Post a Comment

0 Comments