KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ADUWAZWA NA MRADI WA MILIONI 800 MWANAMKE MFUGAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA KATIKA JIJI LA ARUSHA ,AOMBA RAIS SAMIA AMTEMBELEE

 Na Joseph Ngilisho-ARUSHA

 
 

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ali Ussi ametembelea mradi wa sh, milioni 800 wa ufugaji wa ng'ombe wa maziwa unaomilikiwa na mwanamke mjasiriamali,Teddy Sulle katika jiji la Arusha  na kumwomba rais Samia Suluhu hasani kuja kutembelea na kujionea maajabu ya mwanamke huyo.


Aidha aliiomba halmashauri hiyo kuendelea kutenga asilimia kumi ya mapato yake ili kuwapatia mitaji wanawake ambao wamejielekeza kwenye fursa za kiuchumi ikiwemo kumwongezea mtaji mwanamke huyo ili kupanua biashara yake.

Akiongea leo Julai 11,2025 mara baada ya mwenge wa uhuru kutembelea mradi huo wenye ng'ombe zaidi ya 200 uliopo mtaa wa Kirika A,Sombetini,Jijini hapa ,kiongozi huyo wa mbio za mwenge alimpongeza mfugaji huyo na kuongeza kuwa tangia aanze kukimbiza mwenge  ikiwa ni halmashauri ya 96 hakuwahi kuona mradi  kama huo wenye ng'ombe wakubwa wa maziwa wa aina hiyo tangu azaliwe unaomilikiwa na mwanamke.

"Mimi tangu nimeanza kuitembelea Tanzania yote bado sijaikamilisha mpaka sasa nimeshatembea hadi leo hii ni halmashauri  96 kati ya 195 ki ukweli leo nimeona maajabu kwa mama huyu ,nimeona ng'ombe hapa tangia nizaliwe sijawahi kuona ng'ombe wakubwa kama hawa ,kiukweli mama  umeendelea kuweka historia kubwa katika taifa hili"

Ussi alipongeza jitihada za mwanamke huyo kwa kuonyesha uvumilivu na ujasiri wa hali ya juu kwa kufunga ng'ombe wa maziwa ndani ya jiji ,alitoa rai kwa  halmashauri ya jiji la Arusha, kumpatia  mtaji zaidi ili kuboresha biashara yake ikiwemo kupanua eneo la ufugaji.

Aidha  aliiomba kamati ya usalama ya Mkoa kumshawishi rais Samia Suluhu Hasani ili katika ziara zake za kikazi jijini humo aweze kumtembelea mwanamke huyo na kumtia moyo.

"Kiukweli mama huyu ameupa heshima kubwa mwenge wetu wa uhuru na mimi natambua Mheshimiwa rais atakuja kufanya ziara hapa ziwe za kikazi ama kutembea katika mkoa wa Arusha ,ningeiomba kamati ya usalama na mkuu wa wilaya ikiwezekana wamshawishi rais afike kutembelea mradi huu"

Kiongozi huyo wa mbio za mwenge aliwaomba wananchi kuendelea kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yao kwa wivu mkubwa ,kwa  kuiga mfano huo ikiwemo  ufugaji wa mbuzi na kuku jambo litakalosaidia kubadili hali zao za maisha.

"Hapa wanapatikana ng'ombe wa maziwa na nyama sisi wengine tumuunge mkono kwa kununua haya maziwa yanayozalishwa hapa na kwenda kuuza ikiwemo viwandani"

Awali Mmiliki wa mradi huo Teddy Sulle  kupitia risala yake iliyosomwa na mwanaye, alisema kuwa mradi huo ulianza mwaka 2008 akiwa na ng'ombe 6 wa maziwa lakini hadi sasa ana jumla ya ng'ombe wa kisasa wa maziwa wapatao 200.

"Mradi huu ulianza kutekelezwa kwa dhamira iliyojaa maono ukiwa na lengo la kupata suluhisho la upatikanaji wa maziwa katika jiji la Arusha na Tanzania kwa ujumla"

Alisema hadi sasa ni Ng'ombe hamsini pekee wanaokamuliwa kati ya miambili waliopo na kuweza kutoa  maziwa zaidi ya lita 1000 kwa siku kwa wastani kila ng'ombe mmoja kutoa lita 25 hadi 30 kwa siku.

Alisema lengo la mradi ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha maziwa lita 2500 kwa siku kwa kufikisha ng'ombe  wapatao 300.

Alisema lengo lingine la mradi ni kuwa mzalishaji mkubwa wa ng'ombe bora wa maziwa katika mkoa wa Arusha kwa sababu sekta ya mifugo inamchango mkubwa katika lishe ,ajira na fursa za kiuchumi.

"Tunampango wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata bidhaa za maziwa kitakacho gharimu  takribani sh,bilioni1.5"

Alisema mradi huo wa ng'ombe wa maziwa kwa sasa  unathamani ya sh, milioni 800 na ametoa ajira za moja kwa moja kwa watu nane na wengine 35 hunufaika na ajira isiyo rasmi.







Ends.....














Post a Comment

0 Comments