DAKTARI BINGWA AJINYONGA KWA WAYA WA ANTENA MOSHI ,MSONGO WA MAWAZO WATAJWA

DAKTARI BINGWA AJINYONGA MOSHI ,MSONGO WA MAWAZO WATAJWA 

DAKTARI  Magreth Swai, amepoteza maisha, baada ya kudaiwa kujinyonga.

Wananchi wa Kata ya Longuo, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wameshtushwa na kifo cha daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali Teule ya Kibosho iliyoko wilaya ya Moshi , mkoani Kilimanjaro, Magreth Joseph Swai (30), aliyekutwa amejinyonga kwa kutumia waya wa antenna ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi.

Tukio hilo limetokea mnamo Julai  10 2025, majira ya saa 3 usiku, katika eneo la Longuo, ambapo marehemu alijinyonga kwa kufunga waya huo juu ya nondo ya mlango wa chumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Saimon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa chanzo kinachochunguzwa ni msongo wa mawazo uliotokana na matatizo ya afya ya akili yaliyokuwa yakimkabili marehemu.

"Ni kweli tukio hilo limetokea. Marehemu alikutwa amejinyonga kwa kutumia waya wa antenna akiwa chumbani kwake. Uchunguzi wa awali unaonesha alikuwa akisumbuliwa na changamoto za afya ya akili kwa muda mrefu," alisema Kamanda Maigwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kutoka kwa majirani na ndugu, marehemu alianza kuonesha dalili za matatizo ya kisaikolojia takribani miaka minne iliyopita, alipokuwa kwenye mafunzo ya vitendo kama daktari maalum wa watoto.

Marehemu Magreth alikuwa ni daktari mkazi katika kituo cha afya cha Longuo, na anatajwa kuwa mtu aliyekuwa na bidii katika kazi yake licha ya changamoto alizokuwa akikabiliana nazo kimya kimya.

Kwa upande wao, majirani na ndugu wameeleza masikitiko yao, wakitoa wito kwa jamii na serikali kuweka mkazo zaidi kwenye huduma za afya ya akili na ushauri nasaha.

“Tukio hili limetuacha na huzuni. Tulimfahamu kama mtu mtulivu na mchapakazi. Haikuwa rahisi kujua alikuwa na shida kubwa kiasi hiki,” alisema mmoja wa majirani.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kushirikiana na kuwasaidia wale wanaopitia changamoto za afya ya akili kwa kuwahimiza kutafuta msaada wa kitaalamu mapema.

Wataalamu wa afya ya akili wameendelea kuhimiza uwekezaji zaidi katika huduma za afya ya akili, wakibainisha kuwa changamoto hiyo haichagui jinsia, taaluma wala nafasi


Post a Comment

0 Comments