Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
TAASISI ya kulinda na kutetea ustawi wa wanyama,Mkoa wa Arusha (ASPA) imeiomba serikali pamoja na wadau wa wanyama hapa nchini kuongeza jitihada za kukabiliana na ukatili dhidi ya mnyama Punda anayetishia kutoweka hapa nchini kutokana na uwepo wa biashara haramu ya nyama hiyo na wimbi la utoroshaji kwenda nchi jirani.
Rai hiyo imetolewa leo julai 15,2025 na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Livingstone Masija wakati akitoa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa Mkoa qa Arusha,kama wadau wa haki za wanyama na kuomba jitihada zaidi zifanyike katika kunusuru ustawi wa Punda .
Alisema takwimu zinaonesha kuwa takribani punda 150 hutoroshwa kila mwezi kutoka nchini kupitia mpaka wa Namanga kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuwapakia kwenye Malori au kutumia njia ya kuwaswaga kama wanachungwa .
"Tumekutana hapa kujaribu kuangalia ustawi wa Punda kwa ujumla jinsi ambavyo wamekuwa wakiteswa ,kuibiwa na kuchinjwa ili kuboresha faida za Punda kwa ujumla"
Alisema licha ya jitihada za Serikali pamoja na Taasisi mbalimbali zinazotetea ustawi wa wanyama mkoani hapa bado jitihada zaidi zinahitajika ili kukomesha uchinjaji na utoroshaji wa Punda kunakotishia kutoweka kwa mnyama huyo nguvu kazi hapa nchini.
"Punda asionekane kama ni nguvu kazi ya kusaidia watu masikini tu bali hata wenye uwezo,tuangalie faida ya Punda na jinsi gani tufanye ili kuboresha maisha ya Punda kwa ujumla"
Masija aliishukuru serikali kwa kuvifunga viwanda vya kuchinja Punda vilivyokuwa katika Mikoa ya Dodoma na Shinyanga baada ya kuvipatia vibali vya kuchinja punda 30 kwa siku lakini badala yake viwanda hivyo vilichinja hadi Punda 100 kwa siku jambo ambalo lilitishia kutoweka kwa raslimali hiyo.
"Serikali imezuia Biashara ya Punda hapa Nchini lakini bado kuna wimbi la utoroshaji wa wanyama hao kupitia mpaka wa Namanga. Ninachoomba sisi sote tushirikiane kukomesha wimbi hilo"
Hata hivyo alishindwa kufafanua iwapo kampeni yao ya kuzuia utoroshaji iwapo imefanikiwa kwa kiwango gani kukomesha matukio hayo kwa kusema kuwa matukio bado yapo ikiwemo ulaji wa nyama ya punda kwa baadhi ya jamii hapa nchini.
Ends .
0 Comments