WAANDISHI WA HABARI 1200 WAJISAJILI BODI YA ITHIBATI

 By Arushadigtal


WAANDISHI 1,200 wamejisajili kwenye mfumo wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) mpaka jana.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula amesema kwamba leo ndiyo mwisho wa waandishi kujisajili na hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Dirisha la usajili kwenye mfumo wa JAB lilifunguliwa mwezi uliopita na waandishi wanaojisajili wanapata vitambulisho maalumu vitakavyowawezesha kufanya shughuli za kihabari. Leo ndiyo tarehe ya mwisho ya kujisajili.

“Usipojisajili hautaruhusiwa kuchukua wala kuchakata habari, kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za kisheria ambapo adhabu yake ni faini, kifungo jela au vyote kwa pamoja,” alisema Kipangula alipozungumza na gazeti la HabariLEO jana.

Kwa mujibu wa JAB, mwandishi ambaye hatojisajili kwenye mfumo na kupatiwa kitambulisho hatoruhusiwa kuchakata habari zozote zikiwamo za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Wajumbe wa Bodi ya Ithibati

“Natoa wito kwa waandishi wa habari ambao hawajajisajili kwenye mfumo leo (jana), waingie kwenye mfumo kwa wingi kujisajili kwani mfumo unaweza kuhudumia watu wengi kwa pamoja,” alisema Kipangula.

Kuhusu changamoto za waandishi kujisajili, Kipangula alisema: “Tulishatangaza kama kuna anayepata changamoto kujisajili awasiliane na sisi au afike ofisini kwetu kwa usaidizi na watu wengi wamefanya hivyo na wamefanikiwa”.

Kuundwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ni matekelezo ya matakwa ya muda mrefu ya waandishi wa habari walioomba kuwapo kwa bodi hiyo ili kusimamia wanataaluma ya habari kama ilivyo kwa taaluma nyingine.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Tido Mhando alisema kuanzishwa kwake ni hatua muhimu katika mchakato wa kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari kwa kuhakikisha wanahabari wanazingatia viwango vya juu vya weledi, maadili na uwajibikaji.

Tido alisema kuthibitishwa ithibati na bodi kunakuza hadhi na heshima ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama sheria na udaktari, uandishi wa habari unapaswa kutambuliwa rasmi kama taaluma yenye hadhi na umuhimu mkubwa katika jamii. Kupitia ithibati, waandishi wa habari wanapata utambulisho rasmi unaowawezesha kufanya kazi zao kwa heshima na uadilifu,” alisema Tido.

Aliongeza: “Mbali na hayo, waandishi wa habari waliothibitishwa wanaweza kupata unafuu katika kupata habari kutoka kwa taasisi za serikali na sekta binafsi kwa kuwa wanatambulika rasmi”.

Post a Comment

0 Comments