Ad
Breaking🔥

SABGOLD YAWEKA MKAKATI KUWAWEZESHA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU KAHAMA

.. YATAKA DHAHABU IWE DHAMANA YA MIKOPO, YAWALENGA WACHIMBAJI WADOGO

....Yaanzisha mkakati wa kuwapatia mitaji, mashine na kemikali kwa gharama nafuu, yaandaa mfumo wa pointi 2027

Na Joseph Ngilisho | Dar es Salaam

 

KAMPUNI ya Sabgold Refining imekuja na mkakati wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini kupata mitaji, mashine, kemikali na huduma muhimu za migodini, huku ikizitaka taasisi za fedha kutambua dhahabu kama dhamana inayoweza kutumika kupata mikopo ili kuongeza uwezo wao wa kiuchumi.

Mkakati huo unalenga kuondoa vikwazo vinavyowakabili wachimbaji wadogo, ambao licha ya kuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa dhahabu nchini, bado wanakabiliwa na changamoto ya mitaji, upatikanaji wa vifaa na gharama za huduma za migodini.


Kupitia mpango huo, kampuni hiyo inakusudia kubadili mfumo wa mahusiano na wachimbaji wadogo kutoka katika biashara ya kununua dhahabu pekee na kuwa mshirika wa maendeleo yao kwa kuwaunganisha na huduma mbalimbali zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na rasilimali wanazozalisha.



Akizungumza Novemba 21, 2026, katika Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu Mtendaji wa Sabgold Refining, Naasirhussein, alisema kampuni hiyo imejipanga kuwa kiungo muhimu kati ya wachimbaji wadogo na watoa huduma za uchimbaji ili kurahisisha upatikanaji wa mahitaji yao kwa gharama nafuu.

Alisema wachimbaji wadogo ni nguzo muhimu katika sekta ya madini, akibainisha kuwa takribani asilimia 40 ya shughuli za sekta hiyo zinahusisha kundi hilo, hivyo uwezeshaji wao unapaswa kupewa kipaumbele.

"Wachimbaji wadogo wana nafasi kubwa katika ukuaji wa sekta ya madini. Tunahitaji kuwasaidia kupata vifaa, mitaji, kemikali na huduma bora ili waweze kuongeza uzalishaji. Tunapoimarisha uwezo wao, tunakuwa tumeimarisha pia sekta ya madini na uchumi wa taifa," alisema.

Alisema Sabgold Refining, yenye kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichopo Kahama mkoani Shinyanga, imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wachimbaji wadogo na kubaini changamoto zinazowakabili, zikiwamo upatikanaji wa kemikali, mashine na umeme.

Alifafanua kuwa kampuni hiyo pia ni msimamizi rasmi wa dhahabu (Official Custodian) chini ya Mpango wa Serikali wa Ununuzi wa Dhahabu (GDPP) mkoani Kahama, nafasi inayoiwezesha kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mnyororo wa biashara ya dhahabu.

"Katika kipindi hiki tunajiandaa kwenda mbele zaidi kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na wadau wengine kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata mazingira bora ya kufanya shughuli zao, sambamba na malengo ya Dira ya 2030," alisema.

DHAHABU KUWA DHAMANA YA MIKOPO

Katika eneo la upatikanaji wa mitaji, Naasirhussein alitoa wito kwa taasisi za kifedha nchini kuangalia uwezekano wa kutambua dhahabu kama mali inayoweza kutumika kuwa dhamana ya mikopo, hatua aliyosema inaweza kuwafungulia wachimbaji wadogo fursa za kifedha ambazo kwa sasa ni ngumu kuzipata.

Alisema mfumo wa kawaida wa utoaji mikopo unaotegemea zaidi hati za nyumba, viwanja na mali nyingine zisizohamishika unaweza kuwa kikwazo kwa wachimbaji wengi ambao hawana dhamana hizo, licha ya kuwa na dhahabu yenye thamani.

Alisema kutambua dhahabu katika mifumo ya dhamana za kifedha, kwa kuzingatia taratibu za uthamini, umiliki na usalama, kutawawezesha wachimbaji kutumia thamani ya rasilimali wanayozalisha kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao.

"Ni wakati wa kuangalia namna dhahabu yenyewe inavyoweza kuwa dhamana ya mikopo. Mchimbaji anaweza asiwe na nyumba au mali nyingine inayokubalika benki, lakini akawa na dhahabu yenye thamani. Tukiweka mfumo unaotambulika, tunaweza kuwafungulia fursa kubwa za kifedha," alisema.

MFUMO WA POINTI KUANZA 2027

Katika hatua nyingine, Sabgold Refining inapanga kuanzisha mfumo wa pointi mwaka 2027 utakaowapa wachimbaji wadogo wanaouza dhahabu kupitia kampuni hiyo fursa ya kupata huduma na bidhaa mbalimbali kulingana na pointi watakazokusanya.

Naasirhussein alisema mfumo huo utakuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mchimbaji hapati manufaa ya kuuza dhahabu pekee, bali pia anapata fursa ya kurahisishiwa mahitaji mengine muhimu katika shughuli zake za uzalishaji.

Alisema kupitia mfumo huo, wachimbaji watakaokuwa na mahitaji ya kemikali, mashine au huduma nyingine za migodini lakini wakakabiliwa na changamoto ya fedha, wataweza kuunganishwa na kampuni zinazotoa huduma hizo.

"Tunataka mchimbaji anapokuja kuuza dhahabu yake kwetu apate manufaa zaidi ya biashara hiyo. Kupitia mfumo wa pointi, tutaweza kuwaunganisha na kampuni za kemikali na wasambazaji wa vifaa ili wapate huduma kwa gharama nafuu," alisema.

Alisema tayari kampuni imeanza mazungumzo na baadhi ya watoa huduma za migodini ambao wameonyesha utayari wa kushirikiana katika utekelezaji wa mpango huo.

Aliongeza kuwa dhamira yao ni kujenga mfumo utakaowasaidia wachimbaji kupata huduma kwa uwazi, kulinda maslahi yao na kuongeza uwezo wao wa kiuchumi.

KAHAMA NI MWANZO, GEITA NA MUSOMA KUFUATA

Akizungumzia wigo wa utekelezaji, Naasirhussein alisema Sabgold Refining imeanzia Kahama mkoani Shinyanga na hadi sasa imefikia wachimbaji wadogo wapatao 150 hadi 160 kupitia huduma zake.

Alisema kampuni hiyo ina mpango wa kupanua huduma zake katika maeneo mengine yanayozalisha dhahabu, yakiwamo Geita na Musoma, kabla ya kuendelea katika maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa.

Alisema upanuzi huo unalenga kuhakikisha wachimbaji wengi zaidi wanapata huduma zinazohitajika katika shughuli zao, huku kampuni ikiendelea kujenga ushirikiano na wadau wa sekta ya madini.

Alisisitiza kuwa maendeleo ya wachimbaji wadogo hayawezi kutegemea juhudi za kampuni moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa Serikali, taasisi za fedha, kampuni za huduma za migodini na wadau wengine wa sekta hiyo.

Alisema endapo wachimbaji watapata mitaji, vifaa na huduma bora, wataongeza uwezo wa uzalishaji, kuboresha shughuli zao na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta ya madini.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم