ARUSHA KUPATA FLYOVER, BARABARA ZA NJIA NNE KUELEKEA UKUMBI WA KIMATAIFA
...Bodi ya Barabara yapongeza miradi ya miundombinu, kila wilaya yanufaika; Mkoa waungana kuhakikisha maandalizi ya AFCON 2027 yanakamilika kwa wakati
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
ARUSHA inatarajia kupata miundombinu mipya ya kisasa ya usafiri, ikiwemo ujenzi wa barabara za njia nne na daraja la juu (Flyover), katika mpango wa kuunganisha Ukumbi mpya wa Kimataifa wa Mikutano unaojengwa eneo la Kijenge jijini hapa na mtandao wa barabara za jiji hilo.
Mpango huo unatajwa kuwa sehemu ya maboresho makubwa ya miundombinu yanayoendelea kutekelezwa mkoani Arusha, sambamba na maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya barabara na viwanja vya michezo, huku kila wilaya ya mkoa huo ikinufaika na miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
Alisema mpango wa kujenga barabara za njia nne na Flyover, kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, unalenga pia kuboresha muunganiko wa barabara kuelekea ukumbi mpya wa kimataifa wa mikutano unaojengwa Kijenge.
“Tunatarajia kuunganisha ujenzi wa ukumbi huu mpya wa kimataifa wa mikutano na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, ikiwemo barabara za njia nne na ujenzi wa Flyover. Tunafanya hivyo kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na TAMISEMI,” alisema Makalla.
Alisema maendeleo hayo yanaenda sambamba na maandalizi ya AFCON 2027, ambayo yanahitaji miundombinu bora ya barabara, viwanja vya michezo na huduma nyingine ili kurahisisha usafiri wa wageni, mashabiki na wadau watakaofika Arusha.
Alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha changamoto za miundombinu zinapatiwa ufumbuzi na kwamba wananchi wanapata huduma bora kupitia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Tunatambua dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za miundombinu. Kila wilaya ya Mkoa wa Arusha imenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali,” alisema.
Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa ushirikiano na uzalendo wanaouonyesha katika kupisha na kuwezesha utekelezaji wa miradi, hususan ile inayohusiana na maandalizi ya AFCON 2027.
Alisema mafanikio ya maandalizi hayo yanahitaji ushirikiano wa Serikali, viongozi, taasisi na wananchi, akibainisha kuwa Mkoa umejipanga kuhakikisha miradi inayohitajika inakamilika kwa wakati.
MAKONDA, SABAYA WAZUNGUMZIA MIRADI
Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, akieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa maelekezo na miradi inayofanyika mkoani humo.Makonda alisema usimamizi wa karibu wa miradi ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na wananchi wanapata manufaa ya uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya, aliipongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kusimamia miradi mbalimbali ya barabara inayotekelezwa mkoani humo, akisema hatua hiyo imechangia kupunguza changamoto za usafiri na kuboresha mtandao wa barabara.
Sabaya alimpongeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Masawe, kwa jitihada za kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha mtandao wa barabara unaendelea kuboreshwa.
Alisema uwekezaji katika barabara ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na uchumi wa mkoa, kutokana na mchango wake katika kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuunganisha maeneo mbalimbali ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Baraka Messiaky, alimuunga mkono Makalla kwa kusisitiza umuhimu wa usimamizi wa miradi ya maendeleo na ushirikiano wa viongozi katika kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji unaofanywa.
AFCON 2027 NA FURSA ZA ARUSHA
Uboreshaji wa miundombinu ya barabara na ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya mikutano unatarajiwa kuwa sehemu ya maandalizi ya Arusha kukabiliana na ongezeko la wageni na shughuli za kiuchumi zinazoweza kuchochewa na AFCON 2027.
Kwa mkoa unaohudumia shughuli za utalii, biashara na mikutano ya kimataifa, maboresho ya barabara yana umuhimu katika kurahisisha usafiri na kuimarisha muunganiko wa maeneo mbalimbali ya jiji na wilaya zinazouzunguka.
Hata hivyo, Bodi ya Barabara imesisitiza umuhimu wa kufuatilia miradi kwa karibu, kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia fedha zilizotengwa, viwango vya ubora na muda uliopangwa ili maandalizi ya AFCON 2027 yaweze kufanyika kwa mafanikio.
Ends






إرسال تعليق