LUKUMAY: SAMIA AMEIBADILISHA ARUMERU, AORODHESHA MABILIONI YA MIRADI
..Mbunge asema barabara ya kilomita 18, maji na madaraja ni sehemu ya mafanikio ya Serikali – ampongeza Wasira kwa kuwa mlezi wa CCM Arusha
Na Joseph Ngilisho | Arusha
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mageuzi ya maendeleo jimboni humo kupitia uwekezaji katika barabara, maji, madaraja, elimu na umeme, akisema miradi hiyo imeanza kubadili maisha ya wananchi.Lukumay alisema hayo wakati wa mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira, aliyeteuliwa kuwa mlezi wa chama hicho mkoani Arusha, akieleza kuwa ujio wake umeongeza hamasa na kuimarisha ari ya wanachama.
Akizungumza katika mapokezi ya mlezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha ,Steven wasira,na kumpongeza rais Samia kwa serikali kutekeleza wa Ilani ya CCM.
Lukumay alitaja ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 18 kutoka Mianzini hadi Ngaramtoni kuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa jimboni humo.
"Rais Samia ametusaidia sana katika kutatua changamoto za wananchi wetu. Fedha zimetolewa, mabomba yamepelekwa Kiranyi na usambazaji utaendelea katika kata nyingine ili wananchi wapate huduma ya maji,” alisema.
MADARAJA YAFUNGUA MAWASILIANO
Akizungumzia miundombinu ya barabara, Lukumay alisema Serikali imetekeleza ujenzi wa daraja la Oldoro lenye thamani ya Sh milioni 178, ambalo kwa muda mrefu lilikuwa changamoto kwa wananchi.
Alisema pia kuna maandalizi ya ujenzi wa daraja la Muyuni Mnadani lenye thamani ya Sh milioni 150 pamoja na kivuko cha Mwandet kitakachogharimu Sh milioni 69.
Alisema miradi hiyo itasaidia kurahisisha mawasiliano na shughuli za kiuchumi kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kuvuka maeneo hayo.
Katika elimu, alisema Serikali imeendelea kujenga madarasa na kuimarisha utekelezaji wa elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, huku wanafunzi wa elimu ya juu wakiendelea kunufaika na mikopo.
Kuhusu nishati, alisema vijiji vyote vya jimbo hilo vimefikiwa na umeme, huku Serikali ikiendelea na mpango wa kupeleka huduma hiyo katika vitongoji, akitaja maeneo ya Oljoro na Namanyata.
WASIRA APEWA SIFA
Katika hatua nyingine, Lukumay alisema kuteuliwa kwa Wasira kuwa mlezi wa CCM mkoani Arusha ni fursa muhimu ya kuimarisha chama, kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika uongozi.
Alisema Wasira ni kiongozi anayeheshimika na mwenye uwezo wa kuhamasisha wanachama, akitolea mfano wa ziara yake ya Septemba 4, 2025, alipokwenda Arumeru Magharibi kuzindua kampeni yake ya ubunge.
Akizungumzia maelekezo ya Wasira kwa viongozi wa chama, Lukumay alisema msisitizo wa kurejea kwa wananchi, kusikiliza wanachama, kuimarisha uadilifu na kupinga rushwa ni msingi muhimu wa kuimarisha CCM.
Alisisitiza viongozi kuwa wakweli, wawazi, wawe na upendo na wajiepushe na rushwa. Kiongozi lazima ajipime kama anawafaa watu anaowaongoza. Usipowahudumia wananchi kulingana na matarajio yao, hawatakuwa na sababu ya kukuchagua tena,” alisema.
Lukumay aliwataka wakazi wa Arumeru kuendelea kudumisha amani na mshikamano, huku akimwomba Mwenyezi Mungu ampe Rais Samia afya njema ili aendelee kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Ends
Post a Comment