LEMA AFUNGUKA SAKATA LA MARIDHIANO CHADEMA
...Asema hakuwahi kupinga maazimio ya chama, ataka kauli zinazogawa viongozi kukemewa
Na Joseph Ngilisho | Arusha
MBUNGE wa zamani wa Arusha Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, amefafanua msimamo wake kuhusu suala la maridhiano ndani ya chama hicho, akisema hoja anazozitoa zinatokana na maazimio rasmi ya Kamati Kuu ambayo alishiriki kuyatengeneza.Lema amesema Kamati Kuu iliunda kamati ndogo iliyokuwa na jukumu la kutafakari njia za kusonga mbele kufuatia matukio ya Oktoba 2024, ambapo iliazimia kuweka masharti mawili kabla ya kuingia katika mazungumzo ya maridhiano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha Nov 01,2026, Lema alisema sharti la kwanza lilikuwa kuundwa kwa tume huru yenye uwakilishi wa kimataifa, itakayojumuisha watu wenye uwezo na misimamo ya kujitegemea ili kubaini ukweli bila upendeleo.
Alisema sharti la pili lilikuwa kuachiwa huru bila masharti Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
“Nilikuwa mjumbe wa kamati ndogo ya Kamati Kuu iliyotengeneza maazimio hayo. Makamu Mwenyekiti John Heche alipoyasoma hadharani, hayakuwa maazimio yake binafsi, bali yalikuwa maazimio ya chama,” alisema Lema.
Alisema tangu maazimio hayo yatangazwe, vikao mbalimbali vya Kamati Kuu na Sekretarieti vimeendelea kufanyika, lakini suala la maridhiano halijawahi kuwasilishwa kama ajenda rasmi ya majadiliano katika vikao alivyoshiriki.
Lema alieleza kutoridhishwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kuhusu viongozi wa chama hicho, akisema zimekuwa zikijenga taswira ya kutokuwepo kwa mshikamano na kuathiri morali ya wanachama wanaoshiriki katika harakati za chama.
Alitolea mfano kauli iliyodai kuwa viongozi wawili pekee, John Heche na Tundu Lissu, ndio wenye mapungufu, akisema aliona si sahihi kwa viongozi wengine kuachwa nje ya mjadala huo.
“Nilisema kama sisi wengine wote tuna mapungufu, basi yasemwe. Si Heche pekee yake na Lissu pekee yake. Mimi pia nina mapungufu,” alisema.
Alisema kauli hizo zilipaswa kukemewa na viongozi wa chama kwa kuwa zilikuwa na uwezo wa kuibua mgawanyiko kuanzia ngazi za matawi, kata, majimbo, wilaya, mikoa na kanda hadi taifa.
Katika hatua nyingine, Lema alisema amekuwa akipoteza marafiki wengi katika kipindi cha matukio mbalimbali ya kisiasa nchini, akieleza kuwa Arusha na maeneo mengine yameshuhudia vifo vya watu wengi aliowafahamu na kushirikiana nao katika harakati za kisiasa.
ALUTE ALIKUWA MTU WA MISIMAMO
Awali, Lema alitoa pole kwa familia ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kufuatia kifo cha Alute Mughwai Lissu, akisema alifahamishwa kuhusu msiba huo baada ya kupigiwa simu.
Alisema alimfahamu zaidi Alute wakati wa kesi ya rufaa iliyosikilizwa Dar es Salaam, ambapo Tundu Lissu alishirikiana na Wakili Kima Mgoro katika upande wake, na Mahakama ya Rufani kurejesha ubunge wake wa Arusha Mjini.
Lema aliitaja familia ya Lissu kuwa ni familia yenye misimamo thabiti na inayothamini haki, akisema marehemu alikuwa mtu jasiri, makini na mwenye msimamo.
Alisema kifo cha Alute ni pigo kwa familia hiyo, huku akitoa pole kwa ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huo.
Ends..


إرسال تعليق