KADOGOSA AIPA TBA AGIZO ZITO, ITUMIE ARDHI KUJITAJIRISHA
...Aitaka ijikite kwenye biashara, ijenge majengo ya kibiashara na ipunguze utegemezi wa Serikali – Aonya wadaiwa wa kodi, ataka hatua kali dhidi yao
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kungu Kadogosa, ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuachana na mtazamo wa kutegemea kodi za nyumba na fedha za Serikali, badala yake utumie utajiri wa ardhi na majengo inayomiliki kuwekeza katika miradi ya kibiashara itakayoiwezesha kujitegemea kifedha.
Kadogosa alisema TBA ina utajiri mkubwa wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ambao haujatumika kikamilifu, hivyo ni wakati sasa kwa taasisi hiyo kubadili mfumo wa uendeshaji na kujikita katika uwekezaji wenye tija, ikiwemo ujenzi wa majengo ya biashara, maduka na makazi ya kupangisha kwa bei za soko.Alisema hatua hiyo itaiwezesha TBA kuzalisha mapato yake, kupata mitaji ya kuendeleza miradi mipya na kupunguza utegemezi wa Serikali katika kugharamia shughuli zake.
Waziri huyo alitoa maelekezo hayo Nov 24,2026 alipotembelea mradi wa ujenzi wa majengo ya makazi na biashara wa TBA katika eneo la Kaloleni jijini Arusha, ambako alisisitiza kuwa eneo hilo lina thamani kubwa kiuchumi na linapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia fursa zilizopo.Alisema eneo hilo ni mali yenye thamani ya kipekee kutokana na lilipo, hivyo halipaswi kutumiwa kwa mtazamo wa kujenga nyumba za wafanyakazi pekee bila kuzingatia uwezekano wa kuzalisha mapato zaidi.
“Tunataka TBA ianze kufikiria kibiashara. Eneo hili lina thamani kubwa sana, kama lingekuwa madini lisingekuwa dhahabu bali almasi. Kwa hiyo ni lazima tutumie vizuri fursa tulizonazo ili mali hizi zituzalishie fedha,” alisema.
Kadogosa alisema pamoja na wajibu wa TBA kuwapatia wafanyakazi wa Serikali makazi kwa gharama nafuu, taasisi hiyo inapaswa kuchanganya matumizi ya maeneo yake kwa kujenga majengo ya biashara na nyumba nyingine zitakazopangishwa kwa bei za soko.
Alisema nyumba za wafanyakazi zinapaswa kuendelea kutolewa kwa gharama nafuu kwa takribani asilimia 30 chini ya bei ya soko, lakini uwekezaji wa kibiashara uwe sehemu muhimu ya mkakati wa kuongeza mapato.
“Tunataka kuwe na mchanganyiko wa matumizi ya eneo hili. Kuwe na nyumba za wafanyakazi, lakini pia kuwe na biashara na nyumba zitakazopangishwa kwa bei ya soko. Tunahitaji kupata fedha zitakazotuwezesha kujenga maeneo mengine,” alisema.
Alisema TBA inapaswa kutumia mali zake kama msingi wa kupata mikopo katika taasisi za kifedha, badala ya kusubiri Serikali itoe fedha kila inapohitaji kuanzisha mradi mpya.
Kadogosa alieleza kuwa taasisi hiyo inapaswa kuandaa miradi yenye uwezo wa kuzalisha mapato na kuonyesha namna itakavyorejesha mikopo, jambo litakalovutia benki na wawekezaji kushirikiana nayo.
Akizungumzia thamani ya mali za TBA, alisema taarifa alizopewa zinaonyesha kuwa mali za taasisi hiyo katika mikoa 11 zina thamani ya takribani Sh1.45 trilioni, lakini tathmini mpya inayozingatia thamani halisi ya sasa inaweza kufikisha thamani hiyo zaidi ya Sh3 trilioni hadi Sh4 trilioni.
Alisema baadhi ya mali zinaweza kuuzwa kwa utaratibu unaozingatia maslahi ya taasisi ili kupata mitaji ya uwekezaji, huku nyingine zikiendelea kumilikiwa na TBA na kutumika kuzalisha mapato.
Katika hatua nyingine, Kadogosa alisema Serikali inataka sekta binafsi iwe mshirika mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mfumo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Alisema mwelekeo huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kujenga uchumi wa dola trilioni moja, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wake na sekta ya umma asilimia 30.
Alitolea mfano sekta ya barabara, akisema Serikali inaweza kushirikisha wawekezaji katika miradi mikubwa, ikiwemo barabara ya Arusha kuelekea Moshi, pamoja na kutumia mfumo wa hati fungani kupata fedha za ujenzi.
Alisema fedha hizo zinaweza kurejeshwa kupitia mapato yatakayopatikana katika matumizi ya miundombinu hiyo, kwa kuzingatia mifumo ya ushuru itakayowekwa.
Katika hatua nyingine, Kadogosa ameitaka TBA kuimarisha ukusanyaji wa kodi za pango na kuchukua hatua kali dhidi ya wapangaji wanaokaidi kulipa madeni, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kutumia nyumba za Serikali bila kutimiza wajibu wake wa kimkataba.
Alisema tabia ya baadhi ya wapangaji kuchelewesha au kukwepa kulipa kodi inaisababishia taasisi hiyo kukosa mapato yanayostahili na kudhoofisha uwezo wake wa kujiendesha na kuwekeza.
Alielekeza TBA kutumia teknolojia ya Smart Lock kudhibiti matumizi ya nyumba kwa wapangaji wanaokiuka masharti ya malipo, huku akisisitiza kuwa katika maeneo ambayo mfumo huo haujafungwa, hatua zichukuliwe kwa kufuata taratibu za kisheria na mikataba.
Kadogosa alisema wadaiwa wanapaswa kuwasilisha mipango ya kulipa madeni yao, kuanza na malipo ya awali yatakayokubaliwa na kutekeleza ratiba watakayoingia na taasisi hiyo.
Alionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza makubaliano hayo wakabiliwe na hatua za kisheria, ikiwemo kuondolewa katika nyumba wanazokaa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia maelekezo hayo, Mkurugenzi wa TBA, Said Mndeme, alisema taasisi hiyo tayari imeanza operesheni ya kuwashughulikia wapangaji wenye madeni sugu, huku ikidai zaidi ya Sh6 bilioni za kodi ya pango katika maeneo mbalimbali nchini.
Mndeme alisema operesheni hiyo imeanza Dodoma na ndani ya siku tatu imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh250 milioni, hatua ambayo imeipa taasisi hiyo matumaini ya kurejesha mapato yaliyokuwa yamekwama.
Alisema operesheni hiyo itasambazwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, ambako kuna wapangaji wenye madeni makubwa.
“Tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na tayari tumeanza kuyatekeleza. Operesheni hii itaendelea katika mikoa mingine ili kuhakikisha wadaiwa sugu wanalipa madeni yao na mapato ya Serikali yanalindwa,” alisema Mndeme.
Alisema TBA pia itafanyia kazi maelekezo ya Waziri kuhusu mapitio ya mpango wa uendelezaji wa eneo la Kaloleni ili kuongeza matumizi ya kibiashara na kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha mapato yanayolingana na thamani ya eneo husika.
Ends

Post a Comment