EALA YATAKA MKAKATI MPYA WA KULINDA AMANI NA BIASHARA ZA KIKANDA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Onyo hilo limetolewa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Joseph Ntakirutimana, akisema mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani, migogoro ya kivita, mvutano wa kisiasa baina ya mataifa makubwa na kuvurugika kwa mifumo ya usambazaji bidhaa vinaendelea kuleta athari zinazoweza kudhoofisha uchumi wa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema ingawa nchi nyingi za Afrika Mashariki ziko mbali kijiografia na maeneo mengi yanayokumbwa na migogoro ya kimataifa, haziwezi kujitenga na athari zake kwa kuwa uchumi wake umeunganishwa na masoko ya dunia.
Alitaja athari hizo kuwa ni pamoja na kupanda na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, changamoto za upatikanaji wa chakula na nishati, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji pamoja na kutokuwa na uhakika wa mazingira ya biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika ufunguzi wa Semina ya Mahusiano baina ya Mabunge ,inqyofanyika JIJINI Arusha ,Ntakirutimana alisema hali hiyo inapaswa kuwaamsha wabunge wa nchi wanachama kuchukua nafasi yao katika kutengeneza mifumo imara ya kisheria na kisera itakayolinda maslahi ya kiuchumi ya ukanda huo.
Alisema changamoto hizo zinaweka wazi umuhimu wa nchi za EAC kuimarisha biashara baina yake, kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kuziuza, kutafuta masoko mapya na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya kikanda.
"Usalama wa uchumi sasa unazidi kuwa sehemu muhimu ya usalama wa taifa na usalama wa kikanda.
Hatuwezi kuzungumzia amani na usalama bila kuangalia uimara wa uchumi wetu na uwezo wa nchi zetu kujilinda dhidi ya misukosuko inayotokea duniani," alisema.
Alisema nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kujenga uwezo wa kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi badala ya kusubiri athari zitokee ndipo zianze kutafuta suluhisho.
Katika hotuba yake, Ntakirutimana aliwataka wabunge kujiuliza kwa kina sababu zinazoweza kusababisha vita na migogoro ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na namna ya kuizuia kabla haijawa tishio kwa amani na maendeleo ya wananchi.
Alisema ni muhimu kwa viongozi wa kikanda kujenga mifumo ya mapema ya kutambua viashiria vya migogoro, kuimarisha mazungumzo na kuweka utaratibu wa pamoja wa kutatua tofauti zinazoweza kujitokeza baina ya nchi wanachama.
Alisisitiza kuwa Afrika Mashariki haipaswi kuruhusu migogoro inayoweza kuzuilika kugeuka kuwa mapigano yanayoharibu maisha ya wananchi, biashara, uwekezaji na miundombinu ya kiuchumi.
"Ukanda wetu haupaswi kuwa eneo la migogoro. Tunapaswa kujiuliza ni mambo gani yanaweza kusababisha migogoro na vita katika Afrika Mashariki, tunawezaje kuzuia migogoro hiyo na tunapaswa kutumia mifumo gani kupata suluhisho pale inapotokea," alisema.
Aliongeza kuwa majadiliano ya pamoja na ushirikiano wa kisiasa ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazoweza kusaidia nchi wanachama kukabiliana na tofauti zao bila kuathiri mshikamano wa jumuiya.
Kauli hiyo inakuja wakati eneo la Afrika Mashariki likikabiliwa na changamoto za kiusalama, zikiwamo mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya kikanda ya kuimarisha amani na usalama.
Ntakirutimana alisema wabunge wana nafasi kubwa katika kuhakikisha nchi za EAC zinakuwa na sera na sheria zinazowezesha biashara kuvuka mipaka, kulinda viwanda vya ndani na kuimarisha usalama wa chakula.
Alisema kupitia kazi zao za kutunga sheria, kuisimamia Serikali, kuidhinisha bajeti na kuhakikisha uwajibikaji, wabunge wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kujenga mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
Alisema ni wajibu wa wabunge kuhakikisha sera zinazopitishwa zinakuza uzalishaji wa ndani, kuimarisha minyororo ya thamani ya bidhaa na kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa urahisi katika nchi wanachama.
Alisisitiza kuwa kuimarisha biashara ya ndani ya jumuiya kutasaidia kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na vikwazo vya kibiashara, migogoro ya kimataifa na mabadiliko ya mifumo ya biashara duniani.
Alisema hatua hiyo itasaidia pia kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika Mashariki katika soko la kimataifa na kuifanya jumuiya kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Akizungumzia umuhimu wa semina hizo, Ntakirutimana alisema jukwaa la Naivasha limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kibunge na kuchochea maamuzi muhimu yaliyosaidia kuendeleza Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alitoa mfano wa semina iliyofanyika mwaka 2017/2018, ambayo alisema ilichangia kuwepo kwa mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Serikali za nchi wanachama, badala ya majukumu hayo kutokuwa na usimamizi maalumu wa kisiasa katika baadhi ya mifumo ya Serikali.
Pia alisema mijadala iliyofanyika katika semina hizo imechangia kuibua na kuendeleza mipango mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda, ikiwamo michezo inayoshirikisha nchi wanachama.
Alisema mafanikio hayo yanaonesha kuwa semina za Naivasha si mikutano ya kawaida ya kubadilishana mawazo, bali ni jukwaa linaloweza kuzalisha mapendekezo na maamuzi yenye athari katika uendeshaji na maendeleo ya jumuiya.
Alisema kwa miaka mingi, semina hizo zimekuwa zikiongeza ushiriki wa mabunge katika masuala ya EAC na kuimarisha dhamira ya pamoja ya nchi wanachama katika kufikia ustawi wa kiuchumi.
Alisema matarajio yake ni kwamba majadiliano hayo yatazalisha mapendekezo yanayotekelezeka yatakayosaidia kuimarisha uwezo wa EAC kukabiliana na changamoto za kimataifa na kuharakisha azma ya kujenga Afrika Mashariki yenye amani, ustawi na mshikamano.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya jumuiya hayawezi kutegemea juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa mabunge, sekta binafsi na wadau wengine katika kujenga uchumi imara na kulinda amani ya ukanda huo.
Ends

إرسال تعليق