Ad
Breaking🔥

CRDB YATOA VITI NA MEZA 50 KUSAIDIA ELIMU SIHA

CRDB YATOA VITI NA MEZA 50 KUSAIDIA ELIMU SIHA

Na Joseph Ngilisho|SIHA

BENKI ya CRDB imesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na Serikali kuboresha sekta ya elimu nchini baada ya kukabidhi viti na meza 50 kwa Shule ya Sekondari SIHA ONE ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini,Cosmas Sadat alisema msaada huo hauwezi kumaliza changamoto zote zinazokabili sekta ya elimu, lakini ni hatua muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali.

Alisema CRDB inaamini kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali ni muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii, hususan katika elimu.

“Tunatambua kuwa hatua hii haiwezi kuondoa changamoto zote zilizopo, lakini ni sehemu ya suluhisho na uthibitisho wa dhamira yetu ya kushirikiana na Serikali kuboresha sekta ya elimu,” alisema.

Alisema utunzaji wa vifaa hivyo utasaidia kuongeza thamani ya msaada uliotolewa na kuwapa wadau wengine moyo wa kuendelea kushiriki katika kuboresha mazingira ya elimu.

“Samani hizi zimetolewa kwa kujinyima kwa wadau wetu, hivyo ni wajibu wetu kuzitunza ili wanafunzi wanaohitimu waachie wengine wazitumie. Hii itakuwa tija ya msaada huu na kuwapa moyo waliotusaidia kuendelea kufanya hivyo,” alisema.

Aliongeza kuwa CRDB kupitia programu zake, ikiwamo dirisha la Imbeju, inaendelea kutambua umuhimu wa ujumuishi na kuwawezesha wananchi katika makundi mbalimbali ya kijamii.

MKUU wa Wilaya ya Siha Dkt. Christopher Timbuka ameishukuru Benki ya CRDB kwa kutekeleza kwa vitendo maono ya Serikali ya kurejesha tabasamu kwa wananchi wa kata ya Biriri.

Amesema baada ya kukabidhi viti na meza 50 katika shule hiyo imesaidia kumaliza kabisa changamoto ya upungufu uliokuwepo na kutawawezesha wanafunzi kukaa kwa usawa, utulivu na wepesi darasani pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

“wakati shule hii inaanza mwaka 2023 ilikuwa na upungufu mkubwa wa viti na meza na tulihakikisha tunafanikisha kupata viti na meza 218 na leo kuongezewa na CRDB 50 inamaliza kabisa changamoto na wanafunzi 248 atakuwa na meza na kiti chake na kubaki na viti 20 vya ziada, tunawashukuru sana CRDB” amesema Mhe. Dkt. Timbuka.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Bw. Binuru Shekidele amewasihi viongozi wa kata na kijiji cha naibili kwa kushirikiana na Mkuu wa Shule kuhakikisha viti hivyo vinatunza ili viweze kutumika kwa muda mrefu kwa wanafunzi wa Shule hiyo.

Amesema Halmashauri itaendelea kushirikiana na Benki ya CRDB katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi na kuwaletea maendeleo.


ENDS..

Post a Comment

أحدث أقدم