CHONGOLO: HORTILOGISTICA AFRICA KUFUNGUA MASOKO YA DUNIA KWA MAZAO YA TANZANIA
....Asema jukwaa hilo litaunganisha wakulima na wanunuzi wa kimataifa, kuongeza thamani ya mazao na kuvutia uwekezaji katika kilimo cha bustani
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Chongolo alisema jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania katika soko la dunia, kuwaunganisha wazalishaji wa mazao na wanunuzi wa kimataifa, pamoja na kuvutia uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo.
Alisema maonesho hayo yana nafasi ya kuibadilisha sekta ya kilimo kutoka katika mfumo wa kuzalisha na kuuza mazao ghafi kwenda kwenye uzalishaji unaozingatia ubora, teknolojia, uchakataji na mahitaji ya masoko ya kimataifa.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda ya washiriki wa maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya TGT, eneo la Bulka jijini Arusha.Alisema ushiriki wa nchi mbalimbali katika jukwaa hilo unatoa nafasi kwa wakulima, kampuni za kilimo na wafanyabiashara wa Tanzania kujifunza teknolojia mpya, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano ya kibiashara na wadau kutoka masoko mbalimbali duniani.
Alisisitiza kuwa Tanzania inapaswa kutumia fursa hiyo kuongeza ushindani wa mazao yake katika masoko ya nje kwa kuimarisha ubora, viwango vya kimataifa, uzalishaji wenye tija na mifumo ya usafirishaji.
Jukwaa hilo linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho, Novemba 9, 2026, na Makamu wa Rais, Deogratias Ndejembi, likitarajiwa kushirikisha washiriki kutoka takribani nchi 40 na zaidi ya wageni 3,000.
HortiLogistica Africa 2026 limekuja wakati Tanzania ikiendelea kutafuta fursa za kupanua masoko ya mazao ya bustani, yakiwamo parachichi, maua, mboga na matunda, ambayo yana uwezo wa kuongeza mapato ya wakulima na kukuza biashara ya kimataifa.
Katika maonesho hayo, kampuni mbalimbali zimeonesha shughuli zao katika mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji wa miche, kilimo, uvunaji, uchakataji, ufungashaji hadi usafirishaji wa mazao kwenda masoko ya nje.
Miongoni mwa kampuni hizo ni Africado Company Limited ya Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, inayojihusisha na kilimo cha parachichi na kuhudumia wakulima wadogo zaidi ya 2,000 katika Kanda ya Kaskazini.
Mwakilishi wa kampuni hiyo, Vincent Marisha, ambaye ni Meneja wa Africado alisema kilimo cha parachichi ni fursa adhimu kwa vijana kutokana na uwezekano wa kujiajiri katika uzalishaji, upatikanaji wa miche, uvunaji, uchakataji na biashara ya zao hilo.
"Kwa upande wa parachichi, naweza kusema ni fursa adhimu au dhahabu kwa vijana. Wengi sasa wana mwamko wa kulima, na ningependa kuwashauri kuwa kilimo cha parachichi kinalipa," alisema.
Alisema Africado inasaidia wakulima wadogo kwa kuwapatia miche, elimu ya kanuni bora za kilimo na kuwaunganisha na masoko, huku kampuni hiyo ikisafirisha parachichi katika masoko ya Ulaya, Asia na India.
Marisha alisema fursa za kilimo cha parachichi hazipaswi kuishia katika uzalishaji pekee, bali vijana wanapaswa kuangalia pia maeneo ya uchakataji na biashara ili kunufaika na mnyororo mzima wa thamani.
Kwa ujumla, HortiLogistica Africa 2026 inalenga kuifanya Arusha kuwa jukwaa la kuunganisha wazalishaji wa Afrika na masoko ya kimataifa, huku Tanzania ikitafuta nafasi kubwa zaidi katika biashara ya mazao ya bustani duniani.
Ends





Post a Comment