POMBE YAIBUKA KICHOCHEO CHA UKATILI WA KIJINSIA, WANAHABARI WATAKIWA KUCHUKUA HATUA
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
MATUMIZI mabaya ya pombe, dawa za kulevya na tumbaku yametajwa kuwa miongoni mwa vihatarishi vinavyoweza kuchochea vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku wadau wakitaka kuimarishwa kwa elimu ya kinga na ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Vicent alisema bado kuna uhitaji mkubwa wa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya matumizi mabaya ya pombe, dawa za kulevya na tumbaku, pamoja na namna yanavyoweza kuongeza vihatarishi vya migogoro na vitendo vya ukatili katika familia na jamii.
Alisema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuibua mijadala ya kijamii, kutoa elimu ya kinga na kusaidia wananchi kutambua madhara ya matumizi ya vilevi kabla hayajaleta athari kubwa katika maisha yao.
Alisema taarifa za matukio ya ukatili zinapaswa kuchunguzwa kwa kina ili kubainisha mazingira na sababu zinazochangia matukio hayo badala ya kuripoti tukio pekee bila kuangalia mizizi ya tatizo.
“Wanahabari wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii, lakini tunahitaji taarifa zinazogusa pia masuala ya kinga, madhara ya matumizi ya vilevi na namna yanavyoweza kuhusishwa na vitendo vya ukatili,” alisema.
Alisema changamoto nyingine inayowakabili wanahabari ni upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi kutoka kwa taasisi zinazohusika na masuala ya dawa za kulevya, afya na ukatili wa kijinsia.
Alisema hali hiyo inaweza kufanya ukubwa wa tatizo usielezwe ipasavyo kwa jamii, hivyo kuzitaka taasisi husika kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari kwa kutoa taarifa zinazohitajika kwa wakati.
Uzito wa hoja hiyo unaonekana pia katika matokeo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS), uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya.
Utafiti huo umebainisha kuwa asilimia 75 ya wanawake ambao waume au wenza wao hunywa pombe na kulewa mara kwa mara wamewahi kukumbwa na ukatili wa kimwili, kingono au kihisia kutoka kwa wenza wao.
Aidha, asilimia 52 ya wanawake ambao wenza wao hunywa pombe na kulewa mara nyingine wamewahi kukumbwa na aina hizo za ukatili, ikilinganishwa na asilimia 33 ya wanawake ambao wenza wao hawanywi pombe.
Kwa wanawake ambao wenza wao hunywa pombe lakini hawalewi, kiwango hicho kilikuwa asilimia 40.
Takwimu hizo zinaonyesha tofauti kubwa ya viwango vya ukatili kulingana na mwenendo wa unywaji pombe wa wenza, jambo linaloonyesha umuhimu wa elimu kuhusu unywaji hatarishi na athari zake katika mahusiano ya kifamilia.
Hata hivyo, takwimu hizo hazimaanishi kuwa pombe ndiyo sababu pekee ya ukatili, bali zinaonyesha uhusiano unaohitaji kuchunguzwa sambamba na sababu nyingine kama ukosefu wa usawa wa kijinsia, tabia za kutawala mwenza na mitazamo inayohalalisha ukatili.
Mtazamo huo unaendana na maelezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ambalo linataja matumizi mabaya ya pombe kuwa miongoni mwa vihatarishi vinavyohusishwa na vitendo vya ukatili wa kingono na ukatili unaofanywa na wenza wa karibu.
WHO inaeleza kuwa ukatili dhidi ya wanawake unatokana na mwingiliano wa sababu mbalimbali katika ngazi ya mtu binafsi, familia, jamii na mifumo ya kijamii, huku matumizi mabaya ya pombe yakiwa miongoni mwa vihatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano wa ukatili.
Hivyo, wadau wanasisitiza kuwa elimu kuhusu matumizi ya vilevi inapaswa kwenda sambamba na elimu ya haki za binadamu, mahusiano yenye afya, udhibiti wa hasira na namna ya kutatua migogoro bila kutumia nguvu.
Akizungumzia mafunzo hayo, mmoja wa washiriki, Aloyce Mkuya , alisema yamekuwa fursa muhimu ya kuongeza maarifa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, pombe na tumbaku.
Alisema elimu haina mwisho na mafunzo yanayozingatia hali halisi ya jamii yana umuhimu mkubwa kwa wanahabari katika kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha na kuelimisha umma.
Alisema atatumia kalamu yake na maarifa aliyoyapata kuelimisha wananchi, kuibua mijadala yenye tija na kuchochea mabadiliko ya tabia katika jamii.
Alisema wanahabari wana wajibu wa kuwa daraja kati ya wananchi na taasisi zinazoshughulikia masuala mbalimbali ya kijamii, lakini wajibu huo hauwezi kutekelezwa ipasavyo bila kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
“Wanahabari tuna wajibu wa kuelimisha jamii na kutumia kalamu zetu kuchochea mabadiliko. Hata hivyo, tunahitaji ushirikiano wa taasisi zinazohusika ili kupata taarifa sahihi zinazotuwezesha kueleza ukubwa wa changamoto hizi,” alisema Mkufya
Alizitaka taasisi za serikali na mashirika yanayoshughulikia masuala ya afya, dawa za kulevya na ukatili wa kijinsia kuimarisha ushirikiano na wanahabari ili taarifa zinazotolewa kwa umma ziwe na ushahidi na zisaidie wananchi kuchukua hatua.
Wadau wa afya na masuala ya ukatili wanasema mapambano dhidi ya matumizi mabaya ya vilevi yanahitaji kuimarisha kinga, utambuzi wa mapema na upatikanaji wa huduma za matibabu na ushauri kwa watu wenye changamoto za matumizi ya vilevi.
Hatua nyingine ni kuimarisha elimu katika familia, shule na maeneo ya kazi, kutoa huduma za ushauri nasaha, kuwafikia vijana walio katika mazingira hatarishi na kuhakikisha waathirika wa ukatili wanapata ulinzi na msaada unaostahili.
Pia, taasisi zinazohusika zinapaswa kuweka mifumo ya kushirikishana takwimu, kutoa taarifa za mara kwa mara na kuimarisha kampeni zinazolenga kubadili tabia na mitazamo inayohalalisha ukatili.
Kwa upande wa vyombo vya habari, wajibu wake haupaswi kuishia kutangaza idadi ya matukio ya ukatili yanayotokea, bali pia kuchunguza sababu zake, kufuatilia hatua zinazochukuliwa na mamlaka na kuelimisha jamii kuhusu namna ya kuzuia matukio hayo.
Mapambano dhidi ya matumizi mabaya ya vilevi na ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa familia, jamii, serikali, taasisi za afya na vyombo vya habari ili kujenga jamii salama na yenye afya.
Ends





إرسال تعليق