Ad
Breaking🔥

ARUSHA DC YATUNUKU TUZO MASHUJAA WA HENDIBOLI- SHIMISEMITA-2026

ARUSHA DC YATUNUKU TUZO MASHUJAA WA HENDIBOLI

Timu ya halmashauri hiyo yaibuka mshindi wa pili kitaifa SHIMISEMITA, Mbeya

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) imewatunuku vyeti vya heshima pamoja na kombe wanamichezo wake walioiwezesha halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili kitaifa katika mashindano ya michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), yaliyofanyika mkoani Mbeya Agosti mwaka huu.

Hatua hiyo ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wa wanamichezo hao katika kuiwakilisha vyema halmashauri, mkoa wa Arusha na kuipa heshima katika mashindano hayo yaliyoshirikisha halmashauri 177 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Vyeti hivyo na kombe vilikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, katika kikao cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo, ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi, nidhamu na mafanikio yaliyopatikana kupitia michezo.

Katika mashindano hayo, timu ya mpira wa Mikono (HENDIBOLI) ya Arusha DC iliibuka mshindi wa pili kitaifa, matokeo yaliyoiweka halmashauri hiyo miongoni mwa zilizofanya vizuri katika mashindano hayo na kuthibitisha umuhimu wa kuwekeza katika michezo kwa watumishi wa umma.

Akizungumza katika hafla hiyo,Nov 14,2926, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Suleiman Msumi, alisema mafanikio hayo ni ya kujivunia kutokana na ushindani uliokuwepo, huku halmashauri 177 zikishiriki mashindano hayo.

Msumi alisema ushindi huo ni matokeo ya juhudi na kujituma kwa wanamichezo walioamua kuitetea heshima ya halmashauri yao na mkoa wa Arusha katika jukwaa la kitaifa.

Alisema halmashauri imeona ni muhimu kuwatambua wanamichezo hao kwa kuwapatia vyeti vya heshima na kombe, ili kuthamini mchango wao na kuwahamasisha kuendelea kufanya vizuri katika mashindano yajayo.

Mbali na timu ya HENDIBOL halmashauri hiyo pia ilitambua wadau wengine wa michezo kwa kuwatunuku vyeti vya heshima kutokana na mchango wao katika kukuza na kuendeleza michezo.

Hatua hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa kutambua vipaji na juhudi za wanamichezo, huku mafanikio ya Arusha DC yakiwa chachu kwa watumishi wengine kushiriki michezo na kuitangaza halmashauri katika mashindano ya kitaifa.

SHIMISEMITA ni mashindano yanayokutanisha watumishi wa Serikali za Mitaa kutoka halmashauri mbalimbali nchini, yakilenga kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano kupitia michezo.









Ends

Post a Comment

أحدث أقدم