Ad
Breaking🔥

WANAFUNZI 32,957 KUFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE ARUSHA


WANAFUNZI 32,957 KUFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE ARUSHA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WANAFUNZI 32,957 mkoani Arusha wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2026, unaoanza leo Oktoba 19 hadi Novemba 6, huku wasichana wakiwa wengi kuliko wavulana.

Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Elimu Mkoa wa Arusha, Dkt. Vincent Kayombo, amesema kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 15,087 sawa na asilimia 45.8, huku wasichana wakiwa 17,870, sawa na asilimia 54.2.

Amesema idadi hiyo inajumuisha watahiniwa wa shule na wa kujitegemea, huku mitihani hiyo ikifanyika katika shule 280, zikiwemo za Serikali 180 na binafsi 100.

Kwa mujibu wa Dkt. Kayombo, idadi ya watahiniwa waliosajiliwa ni sawa na asilimia 84.9 ya wanafunzi 38,826 walioandikishwa kuanza Kidato cha Kwanza mwaka 2023.

Amesema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika, yakiwemo mafunzo elekezi kwa wasimamizi na maandalizi ya watahiniwa kitaaluma, kiakili na kisaikolojia.

“Watahiniwa wameandaliwa vizuri na ninawatakia kila la kheri katika mtihani wao. Ninawasihi wawe watulivu, wajiamini na kumtanguliza Mwenyezi Mungu wakati wote wa mitihani,” amesema Dkt. Kayombo.

Aidha, amewataka wasimamizi kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za mitihani ya Taifa, akisisitiza umuhimu wa kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha uadilifu wa mitihani hiyo.

Amesema wasimamizi wanapaswa kutambua dhamana waliyopewa na Serikali, kwa kuwa usimamizi wao una mchango mkubwa katika kulinda haki za watahiniwa na mustakabali wa elimu nchini.

Dkt. Kayombo amewatakia watahiniwa wote mafanikio mema, akieleza kuwa ufaulu mzuri utawasaidia kutimiza ndoto zao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post