Ad
Breaking🔥

MAOFISA 39 WA MAGEREZA WAPANDISHWA VYEO

MAOFISA 39 WA MAGEREZA WAPANDISHWA VYEO

Na Wdrs Irine Nkana | DODOMA

JESHI LA MAGEREZA limewapandisha vyeo Maofisa 39, wakiwemo Naibu Makamishna 17 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi 22, katika hatua inayolenga kuimarisha uongozi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo.

Vyeo hivyo vimevalishwa leo, Oktoba 19, 2026, na Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP), Jeremiah Yoram Katungu, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato, jijini Dodoma.



Akizungumza katika hafla hiyo, Katungu alimshukuru Rais kwa kuendelea kuliwezesha jeshi hilo kwa kujaza nafasi za uongozi, kuboresha stahiki za watumishi na kutoa vibali vya ajira.

Alisema kupandishwa vyeo kwa idadi hiyo ya maofisa ni tukio la kihistoria kwa jeshi hilo, akiahidi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, nidhamu na ufanisi.

Katungu aliwataka maofisa waliopandishwa vyeo kutumia nafasi zao mpya kuongeza bidii, uwajibikaji na ufanisi katika kusimamia majukumu ya Jeshi la Magereza.

Alisema majukumu hayo ni pamoja na kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata hifadhi salama, kutekeleza programu za urekebu kwa lengo la kuwasaidia kubadilika kitabia na kutoa ushauri kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia uhalifu.

Kwa upande wake, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza (CP), Nicodemus Tenga, aliwataka maofisa hao kuhakikisha wanatekeleza mikakati na maelekezo ya Serikali kwa vitendo, huku wakizingatia sheria, taratibu na miongozo ya jeshi hilo.

Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya utumishi, nidhamu na uwajibikaji ili kuhakikisha majukumu ya Jeshi la Magereza yanatekelezwa kwa ufanisi.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post