WAMAASAI WAKABIDHIWA EKARI 23 BAADA YA MGOGORO WA MIAKA 10
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
JAMII ya Wamaasai imekabidhiwa eneo lenye ukubwa wa ekari 23 na kampuni ya Burka Coffee Estate, lililopo Kata ya Elerai jijini Arusha, kwa ajili ya shughuli za kimila na kuhifadhi urithi wa utamaduni wa jamii hiyo, baada ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 kumalizika.Makabidhiano hayo yaliyoshuhudiwa na viongozi wa Serikali na jamii za Wamaasai ni hatua muhimu katika kuimarisha amani, kuheshimiana na kulinda maeneo yenye umuhimu wa kihistoria na kimila.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,leo Oktoba 16,2026,RC Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amezitaka pande zote kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na kuhakikisha taratibu za kisheria za umiliki wa eneo hilo zinakamilishwa bila vikwazo.Makalla amesisitiza kuwa utatuzi wa mgogoro huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan unapaswa kuwa mwanzo wa utekelezaji wa makubaliano, akionya kuwa Serikali haitarajii kuona suala hilo likikwama tena.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mazungumzo na ushirikiano wa viongozi wa jamii, Serikali na wadau wengine, akiwataka wananchi kuheshimu sheria za nchi, Katiba na utamaduni wa kila jamii.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Viongozi wa Maasai Tanzania (MARYA) – Oreteti Loongaik, Laigwanani Amani Lukumay, amesema eneo hilo litasaidia kuhifadhi mila, desturi, lugha, nyimbo za asili na maarifa ya jadi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Baraza hilo limetoa wito kwa Serikali kupitia wizara yenye dhamana ya utamaduni kushirikiana na viongozi wa Wamaasai kuhakikisha eneo hilo linapata hati miliki na kulindwa kisheria ili litumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Aidha, Lugangira amewataka viongozi wa kimila kushirikiana na Serikali kuendeleza utalii wa utamaduni na kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki ya elimu, akisisitiza umuhimu wa kupinga ndoa za utotoni na mila zinazoweza kuzuia maendeleo ya jamii.
Eneo hilo linatarajiwa kuwa kituo cha kihistoria cha urithi wa utamaduni wa Wamaasai, kitakachosaidia kuhifadhi historia yao, kuendeleza maarifa ya jadi na kukuza utalii wa utamaduni.
Ends..












إرسال تعليق