Ad
Breaking🔥

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI PINGAMIZI LA SERIKALI KESI YA LISSU

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI PINGAMIZI LA SERIKALI KESI YA LISSU

Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkuu wa Gereza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika Shauri la Kikatiba Na. 7300 la mwaka 2026, lililofunguliwa na mawakili wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, wakipinga vikwazo vya kuonana na mteja wao gerezani na kuingiliwa kwa faragha ya mawasiliano yao ya kisheria.

Uamuzi huo umetolewa leo na jopo la majaji watatu linalosikiliza shauri hilo, likiongozwa na Jaji Amir Mruma, akisaidiwa na Jaji Dkt. Angelo Rumisha na Jaji Dkt. Evaristo Longopa.

Shauri hilo lilifunguliwa na mawakili wa Lissu, Maduhu William, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, wakilalamikia kuwepo kwa vikwazo vinavyoathiri uwezo wao wa kuonana na mteja wao akiwa gerezani, pamoja na faragha ya mawasiliano na mashauriano yao ya kisheria.

Katika pingamizi lao, Mkuu wa Gereza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walidai kuwa shauri hilo halikustahili kusikilizwa kutokana na kuwepo kwa njia nyingine za kisheria ambazo waleta maombi wangeweza kuzitumia kupata nafuu, badala ya kufungua shauri la kikatiba.

Hoja hiyo ya serikali ilijengwa katika Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, Sura ya 3, Toleo la mwaka 2023, wakidai kuwa shauri hilo lilikuwa na dosari za kisheria.

Hata hivyo, jopo hilo la majaji limezikataa hoja hizo, likibainisha kuwa Lissu na mawakili wake hawakuwa na njia nyingine mbadala ya kupata haki na nafuu ya kisheria nje ya kufungua shauri hilo la kikatiba.

Kutupiliwa mbali kwa pingamizi hilo kunaondoa kikwazo cha awali kilichowekwa na upande wa serikali dhidi ya shauri hilo.

Baada ya uamuzi huo, Jaji Mruma ameendelea kusoma uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu hoja za msingi zilizowasilishwa katika shauri hilo la kikatiba.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم