UKUMAY AANZA MPANGO MKUBWA WA AFYA YA KINYWA, MENO ARUMERU
• Kliniki ya kinywa na meno kuanza Januari 2027
• Wataalamu Tanzania kwenda Ujerumani kupata mafunzo na uzoefu
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lembulung Lukumay, ameanza mpango wa uwekezaji katika huduma za afya ya kinywa na meno kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha, huku kliniki maalumu ikitarajiwa kuanza kutoa huduma Januari 2027.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Dkt Lukumay kufanya kikao jijini Berlin, Ujerumani, jana Oktoba 1, 2026, na Mkurugenzi wa DENTOGLOBAL, Dkt Ursula Subier, ambapo pamoja walijadili utekelezaji wa mpango huo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
Kwa mujibu wa mpango huo, kliniki ya kinywa na meno itakayoanza Januari 2027 itakwenda sambamba na huduma za kliniki tembezi, zitakazofika katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Arumeru Magharibi, kwa lengo la kuwafikishia wananchi huduma hizo karibu na maeneo wanayoishi.
Dkt Lukumay alisema mpango huo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya kinywa na meno, pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma za kitaalamu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Mbali na utoaji wa huduma, mpango huo unatarajiwa kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania, ambapo baadhi ya wataalamu wa afya ya kinywa na meno watapatiwa nafasi ya kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya mafunzo na kupata uzoefu wa kimataifa katika sekta hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ujuzi na uwezo wa wataalamu hao ili waweze kutumia uzoefu watakaoupata katika kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini, hususan katika Mkoa wa Arusha.
Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa DENTOGLOBAL ya Ujerumani, wadau wa maendeleo wa Ujerumani, Serikali ya Ujerumani, pamoja na TATIC Company na NEPT za Tanzania, Serikali ya Tanzania na wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi.
Mpango huo unaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya kwa wananchi kupitia ushirikiano kati ya Serikali, wabunge, sekta binafsi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.
Ends



إرسال تعليق