Ad
Breaking🔥

TAZAMA PICHA PADRI AFARIKI DUNIA KWA KUANGUKIWA NA MSALABA AKIHUDUMIA MISA

PADRI AFARIKI DUNIA BAADA YA KUANGUKIWA NA MSALABA AKIHUDUMIA MISA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA DIGITAL

PADRI wa Kanisa Katoliki, Patricio Alfredo Sánchez Molinari, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na msalaba mkubwa wa mbao wenye sanamu ya Yesu Kristo alipokuwa akiendesha Misa Takatifu nchini Ecuador.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Jumamosi, Oktoba 17, 2026, katika Kanisa la Nuestra Señora del Perpetuo Socorro, jijini Guayaquil, na kusababisha taharuki miongoni mwa waumini waliokuwa wakishiriki ibada hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa, padri huyo alikuwa akiongoza misa iliyokuwa ikirushwa mubashara kupitia mitandao ya kijamii wakati msalaba uliokuwa ukining’inia ukutani nyuma ya madhabahu ulipojitoa ghafla na kumwangukia.

Tukio hilo lilinaswa katika matangazo hayo, huku waumini wakisikika wakipiga mayowe na kukimbilia eneo la madhabahu kujaribu kumsaidia padri huyo.

Jimbo Kuu Katoliki la Guayaquil limethibitisha kifo cha Padri Sánchez Molinari kupitia taarifa rasmi, likieleza masikitiko yake kutokana na msiba huo na kutoa pole kwa familia ya kidini ya Redemptorists, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.

Padri Sánchez Molinari alikuwa paroko wa kanisa hilo na mwanachama wa Shirika la Redemptorists, linalojihusisha na huduma za kiroho na uinjilishaji. Misa zake zilirushwa pia kupitia mitandao ya kijamii ili kuwafikia waumini wengi zaidi.

Hadi taarifa za awali zilipochapishwa, sababu za msalaba huo kujitoa ukutani hazikuwa zimeelezwa rasmi, huku kukiwa hakuna maelezo ya kina kuhusu hatua za matibabu alizopatiwa kabla ya kuthibitishwa kwa kifo chake.

Kifo cha padri huyo kimeibua huzuni miongoni mwa waumini, huku video ya tukio hilo ikisambaa katika mitandao ya kijamii.




Ends

Post a Comment

أحدث أقدم