TANZANIA NA UGANDA ZAPIGA HATUA KIWANDA CHA KUSAFISHA MAFUTA.
Na Hadija Bagasha|TANGA
TANZANIA na Uganda zimepiga hatua nyingine katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati, baada ya Kamati ya Pamoja ya Ufundi ya nchi hizo kukutana Chongoleani, Tanga, kwa ajili ya kukabidhi eneo litakalojengwa miundombinu ya kupokelea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta yaliyosafishwa.Hatua hiyo imefungua ukurasa mpya katika azma ya kuifanya Tanga kuwa kitovu muhimu cha shughuli za mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku ikitarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi, ajira na fursa za biashara katika mji huo na maeneo yanayouzunguka.
Makabidhiano hayo yamefanyika kati ya Kamati ya Pamoja ya Ufundi ya Tanzania na Uganda na Mshauri Mwelekezi kutoka kampuni ya Worley Consulting Group Limited, ambaye sasa anatarajiwa kuanza kazi za awali za kitaalamu zinazohusisha upembuzi yakinifu wa eneo hilo.
Miongoni mwa kazi zitakazofanyika ni pamoja na upimaji wa udongo, tathmini ya mazingira pamoja na usanifu wa awali wa miundombinu inayotarajiwa kujengwa.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda katika kuendeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na kutumia fursa zinazotokana na uwepo wa miundombinu ya bomba la mafuta ghafi la EACOP.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mradi, miundombinu hiyo inayopangwa kujengwa Chongoleani inatarajiwa kuongeza thamani katika mnyororo wa mafuta, pamoja na kuwezesha shughuli za kupokea, kuhifadhi na kusafirisha bidhaa za petroli kwa ufanisi zaidi.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuchangia katika kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mafuta yaliyosafishwa, kuimarisha usalama wa upatikanaji wa bidhaa za petroli na kuongeza fursa za biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Kamishna Msaidizi wa Mkondo wa Kati na Chini wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati, Grace Mwakasege, amesema mradi huo ni wa kimkakati na una uwezo wa kuifanya Tanga kuwa kituo muhimu cha shughuli zinazohusiana na mafuta na gesi katika ukanda huo.
Mwakasege amesema uwepo wa miundombinu hiyo utaongeza umuhimu wa Tanga katika mnyororo wa thamani wa sekta ya nishati, huku ukiweka mazingira ya kuvutia shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazohusiana na mafuta na gesi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini ya Uganda, Mhandisi Geofrey Ogwang, amesema ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa zaidi kwa wananchi, ikiwamo ajira, uhamishaji wa teknolojia na kukuza shughuli za kiuchumi.
Ogwang amesema wananchi wa Chongoleani na Tanga kwa ujumla wanaweza kunufaika na shughuli zitakazozalishwa na uwekezaji huo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Tanzania na Uganda katika kutekeleza miradi ya nishati yenye manufaa kwa nchi zote mbili.
TANGA YAFUNGUKA KIMKAKATI.
Kwa Tanga, utekelezaji wa mradi huo unaongeza uzito wa nafasi ya mji huo katika ramani ya miundombinu ya nishati ya Afrika Mashariki.
Eneo la Chongoleani tayari limekuwa na umuhimu mkubwa katika mipango ya usafirishaji wa mafuta kupitia bomba la EACOP, na kuongezwa kwa miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta yaliyosafishwa kunaweza kuongeza shughuli za kiuchumi zinazohusiana na sekta hiyo.
Mbali na manufaa ya moja kwa moja katika sekta ya nishati, mradi huo unaweza kuchochea mahitaji ya huduma mbalimbali, ikiwamo usafirishaji, ujenzi, huduma za kitaalamu na biashara zinazohusiana na shughuli za mafuta.
Kwa hatua ya sasa, kinachofuata ni kazi za kitaalamu za upembuzi yakinifu na usanifu, ambazo zitatoa msingi wa hatua zinazofuata za utekelezaji wa mradi.
Hatua hiyo inaashiria namna ambavyo ushirikiano wa Tanzania na Uganda unavyoendelea kubadili fursa za nishati kuwa miradi yenye uwezo wa kuunganisha biashara, uwekezaji na shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Iwapo utekelezaji utaendelea kwa hatua zilizopangwa, Chongoleani inaweza kuwa sehemu muhimu zaidi ya mtandao wa miundombinu ya nishati wa Afrika Mashariki, huku Tanga ikizidi kujijenga kama kituo cha shughuli za nishati na biashara za kimkakati.
Mwisho.



إرسال تعليق