PARESO, LUKUMAY KUIKABA SERIKALI FIDIA ILKIDING’A
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Alisema hatua zilizochukuliwa na uongozi wa shule, bodi, Diwani wa Kata ya Ilkiding’a na Halmashauri zimeonyesha kuwa sehemu kubwa ya wajibu wao imetekelezwa, hivyo kinachohitajika sasa ni Serikali kuwezesha fedha za fidia ili familia hizo zihame na eneo hilo litumike kwa maendeleo ya shule.
Akizungumzia maendeleo ya shule hiyo, Pareso aliipongeza Ilkiding’a kwa hatua iliyopiga tangu kuanzishwa kwake mwaka 1967, ikiwa na wanafunzi 80 na walimu saba, hadi sasa kuwa kituo kikubwa cha elimu chenye takriban wanafunzi 1,400. The
Pia aliipongeza shule hiyo kwa kuongeza ufaulu, akibainisha kuwa katika matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2025, ufaulu ulifikia asilimia 67, huku Kidato cha Pili ukifikia asilimia 87.
Alisema Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwamo madarasa, mabweni, nyumba za walimu na upatikanaji wa teknolojia na intaneti, hatua zinazolenga kuwawezesha wanafunzi kushindana katika dunia ya teknolojia.
Akizungumza na wahitimu, Pareso aliwataka kutumia elimu waliyoipata kama msingi wa hatua nyingine za maisha na kuendelea kujituma katika masomo yao, akisema mahafali hayo ni hatua muhimu katika safari yao ya elimu.
"Nimelichukua jambo hili kwa uzito na nitashirikiana na Mbunge wetu wa Jimbo, Dkt Lukumay, pamoja na wabunge wenzangu wa Mkoa wa Arusha, kulisukuma jambo hili ili Serikali ifanye kazi kwa haraka,” alisema Pareso.
Ahadi hiyo inakuja wakati shule hiyo ikiwa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio, jambo ambalo limehusishwa na uwepo wa baadhi ya wananchi ndani ya eneo linalohitajika kwa matumizi ya shule.
DIWANI AILILIA UZIO
Diwani wa Kata ya Ilkiding’a aliiomba Serikali kusaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa uzio katika shule hiyo, akisema hali hiyo imekuwa ikiathiri usalama wa wanafunzi na mali za shule.
Alisema eneo la shule liko wazi kiasi kwamba mtu anaweza kuingia hadi kwa gari na kufikia maeneo yenye mali za wanafunzi na walimu.
“Si kwamba tumeshindwa kuweka uzio. Changamoto kubwa ni baadhi ya wananchi ambao familia zao zimeishi ndani ya eneo la shule. Tunaomba Serikali itusaidie kuwawezesha wananchi hao kuhamishwa ili tuweze kuweka uzio,” alisema.
Alisema ukosefu wa uzio pia umekuwa ukisababisha changamoto wakati wa mvua, ikiwamo maji kuingia katika eneo la shule na kuongeza hofu kwa baadhi ya wazazi.
PARESO ATOA AHADI KWA WALIMU
Mbali na suala la fidia, Pareso aliahidi kufuatilia changamoto ya upungufu wa walimu, hususan wa masomo ya sayansi, akisema shule hiyo inapaswa kupewa kipaumbele katika mchakato wa ajira na upangaji wa walimu.
Alisema atashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha pengo la walimu linazibwa ili wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunza na kuongeza kiwango cha ufaulu.
Aidha, Pareso aliahidi kushirikiana na uongozi wa shule, Halmashauri na wadau wengine katika kutatua changamoto za ofisi ya walimu, chakula cha mchana, gari la shule na mashine ya fotokopi.
Katika hatua nyingine, Pareso aliahidi kuchangia katika upatikanaji wa mashine ya fotokopi kwa shule hiyo, huku akiwataka wazazi na wadau wengine kuendelea kushirikiana na uongozi wa shule kuboresha mazingira ya elimu.
ILKIDING’A YAKUA
Akizungumzia maendeleo ya shule hiyo, Pareso aliipongeza Ilkiding’a kwa hatua kubwa iliyopiga tangu kuanzishwa kwake mwaka 1967 ikiwa na wanafunzi 80 na walimu saba, hadi sasa kuwa shule kubwa yenye zaidi ya wanafunzi 1,400.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilkiding’a, Sunday Joseph, alisema kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 1,492 na walimu 51, huku ikiwa bado inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na Hisabati.
Alisema shule inahitaji walimu wawili wa Fizikia, wawili wa Kemia, wawili wa Baiolojia na watatu wa Hisabati.
Sunday alisema shule imekuwa ikitumia mikakati mbalimbali kuongeza ufaulu, ikiwamo mitihani ya majaribio, mitihani ya ndani, Mock na mitihani ya pamoja ya shule za Kanda ya Kaskazini Magharibi zinazohusisha Arusha na Manyara.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2025, wanafunzi 16 walipata Daraja la Kwanza, 52 Daraja la Pili, 66 Daraja la Tatu na 96 Daraja la Nne, huku masomo ya Kemia na Fizikia yakifikisha ufaulu wa asilimia 100.
Aidha, alisema shule hiyo ilipata ufaulu wa asilimia 87 katika mtihani wa upimaji wa Kidato cha Pili mwaka 2025.
WAHITIMU 388 WAAGWA
Katika mahafali hayo, Shule ya Sekondari Ilkiding’a iliwaaga rasmi wahitimu 388 wa Kidato cha Nne, ambao ni sehemu ya wanafunzi 556 walioanza Kidato cha Kwanza mwaka 2023.
Sunday alisema baadhi ya wanafunzi walishindwa kuendelea na masomo katika shule hiyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo changamoto za kiafya na wengine kuhamia shule nyingine za Serikali au binafsi.
Alisema pamoja na mafanikio hayo, shule bado inahitaji mashine ya kisasa ya fotokopi yenye thamani ya takribani Sh milioni 13.5, ujenzi wa ofisi ya walimu pamoja na upatikanaji wa chakula cha mchana kwa baadhi ya wanafunzi wa kutwa.
LAIZER: TUNALENGA KUFUTA ZERO
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Afisa Elimu Taaluma, Meijo Laizer, alisema Halmashauri inaendelea kuweka juhudi kuhakikisha shule hiyo inaendelea kuimarika kitaaluma.
Laizer alisema changamoto zilizowasilishwa na shule, ikiwamo suala la uzio na wananchi wanaoishi katika eneo la shule, zimepokelewa na hatua zinaendelea kuchukuliwa.
“Nina uhakika mwaka huu tutakuwa na Zero. Tunapambana kuhakikisha mambo yanaenda vizuri na matokeo ya shule hii yanazidi kuimarika,” alisema Laizer.
Akizungumza na wahitimu, Pareso aliwataka kutumia elimu waliyoipata kama msingi wa hatua nyingine za maisha, kuendelea kujituma na kujiwekea malengo ya elimu na maisha yao ya baadaye.
Alisema mafanikio ya Ilkiding’a ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali, walimu, wazazi, bodi ya shule na wadau wa elimu, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana ili shule hiyo iendelee kupiga hatua.
Ends






















إرسال تعليق