TAMISEMI KUTUMIA MAONI YA VIJANA KUPANGA BAJETI ZA AFYA SERIKALINI- SHEMDOE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imewataka vijana washiriki kikamilifu katika kupanga mipango na bajeti za afya, ikisisitiza kuwa maoni yao lazima yatafsiriwe kuwa hatua za vitendo zitakazoboresha huduma za afya ya uzazi, afya ya akili na huduma rafiki kwa vijana nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, alisema ushiriki wa vijana hautakiwi kuishia katika majadiliano, bali mapendekezo yao yanapaswa kuingizwa kwenye mipango na bajeti za Serikali na kupewa muda maalumu wa utekelezaji.
Alitoa kauli hiyo jijini Arusha , Oktoba 23, 2026, wakati akifungua mkutano wa mazungumzo ya vijana unaoongozwa na vijana na kuhusisha wizara mbalimbali, ulioandaliwa na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA Health Community).
“Ni vyema sisi kama TAMISEMI, ambao tunasimamia vituo hivi vya afya ya msingi, tukawasikiliza vijana na mapendekezo yao ili tuweze kuyaingiza katika mipango na bajeti zetu na kwenda kuyatekeleza,” alisema.
Prof. Shemdoe alisema TAMISEMI ina nafasi muhimu katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili vijana zinapatiwa ufumbuzi, kwa kuwa huduma nyingi za afya wanazotegemea hutolewa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zinazosimamiwa na halmashauri.
Alisisitiza kuwa mapendekezo ya vijana yanapaswa kuwa na hatua mahsusi, muda wa utekelezaji na vigezo vya kupima mafanikio, ili kuhakikisha majadiliano yanazaa matokeo yanayoonekana katika jamii.
Waziri huyo alionya dhidi ya kuzingatia mahitaji ya wasichana pekee katika mipango ya afya ya uzazi, akisema wavulana nao wanakabiliwa na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kujenga familia bora na jamii yenye afya.
Alisema vijana wa kiume na wa kike wanapaswa kuhusishwa kwa usawa katika mijadala na maamuzi yanayohusu afya ya uzazi, huku huduma zikiandaliwa kwa kuzingatia mahitaji yao halisi.
“Tunapotaka kuwa na familia bora hapo baadaye, tunapaswa kuangalia vijana wa kiume na wa kike. Hatupaswi kujikita katika ajenda ya mtoto wa kike pekee,” alisisitiza.
Mkutano huo umewakutanisha takribani vijana 200 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajili ya kujadili afya ya uzazi, afya ya akili, ajira na nafasi yao katika juhudi za kupunguza vifo vya kina mama na watoto.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Health Community, Dkt. Ntuli Kapologwe, alisema mkutano huu umeJumuiya vijana takrinani 200 kutola mikoa yote Tanzania ,ni sehemu ya juhudi za kikanda za kuhakikisha mapendekezo yanayotolewa na vijana yanatekelezwa katika nchi wanachama.
Alisema jumuiya hiyo iliandaa mkutano wa kikanda nchini Eswatini Februari mwaka huu, ulioshirikisha nchi 20 na kutoa nafasi kwa vijana kujadili changamoto zao na kupendekeza maboresho katika huduma za afya na fursa za maendeleo.
Mkutano wa Arusha ni mwendelezo wa majadiliano hayo baada ya mikutano ya awali kufanyika Eswatini na Uganda, ukiwa na lengo la kuimarisha ushiriki wa vijana katika maamuzi yanayohusu afya na maendeleo yao.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Charles Mkomba Chepa, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Dr Grace Maghembe alisema upatikanaji wa huduma bora, salama na nafuu kwa wanawake, watoto na vijana unahitaji kuimarisha vituo vya afya kwa watumishi wenye ujuzi, dawa, vifaa tiba na mifumo madhubuti ya rufaa.Alisema licha ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha huduma za afya, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao kwa wakati, hususan wajawazito, watoto wachanga na vijana.
Alisisitiza pia umuhimu wa kulinda faragha za vijana wanapofika vituo vya afya, kuwapatia ushauri sahihi na kuhakikisha hawanyanyapaliwi kutokana na changamoto zinazowakabili.
Prof.Shemdoe aliongeza kuwa Serikali imewekeza katika miundombinu ya afya ya msingi, hivyo ni wajibu wa mamlaka husika kuhakikisha vifaa na majengo hayo vinatumika kwa ufanisi na kutunzwa ili viendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema mapendekezo yatakayowasilishwa na vijana yanatarajiwa kusaidia kuboresha mipango na matumizi ya bajeti za afya katika ngazi za halmashauri, huku afya ya akili na huduma za afya ya uzazi zikipewa uzito unaostahili.
Ends.









Post a Comment