Ad
Breaking🔥

CRCEG YATULIZA MGOMO MKICC, YASEMA MISHARA IMELIPWA

CRCEG YATULIZA MGOMO MKICC, YASEMA MISHARA IMELIPWA

...Kampuni yafafanua chanzo cha ucheleweshaji, yaomba radhi wafanyakazi

ARUSHA, Oktoba 23, 2026

KAMPUNI ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG), inayojenga Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mount Kilimanjaro (MKICC) jijini Arusha, imesema changamoto ya kuchelewa kwa mishahara iliyosababisha wafanyakazi kusimamisha kazi kwa muda imetatuliwa, huku shughuli za ujenzi zikiendelea.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Oktoba 23, 2026, kampuni hiyo imesema ucheleweshaji wa mishahara iliyopaswa kulipwa Oktoba 20, mwaka huu, ulitokana na hitilafu za kiufundi katika mifumo ya miamala kati ya kampuni na taasisi za kifedha zilizohusika na malipo.

CRCEG imefafanua kuwa hali hiyo haikutokana na kusitisha wajibu wake wa kuwalipa wafanyakazi, ikieleza kuwa baada ya changamoto hiyo kushughulikiwa, wafanyakazi wameanza kupokea stahiki zao na kazi za ujenzi zimeendelea.

Kampuni hiyo imeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza, huku ikiahidi kuimarisha mifumo na uratibu wa malipo ili kuzuia changamoto kama hiyo kujirudia.

Pia imeeleza kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo, ikisisitiza dhamira yake ya kuzingatia sheria za kazi za Tanzania na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

CRCEG imesema inatambua mchango wa wafanyakazi, hususan vijana wa Kitanzania, katika kutekeleza mradi huo wa kimkakati unaotarajiwa kuongeza uwezo wa Arusha kuwa kitovu cha mikutano ya kimataifa na utalii wa biashara.



Aidha, kampuni hiyo imetoa shukrani kwa wafanyakazi, Serikali kupitia taasisi husika ikiwamo PSSSF, uongozi wa Mkoa wa Arusha na wadau wengine kwa ushirikiano wao katika kutatua changamoto hiyo.

Taarifa hiyo inafuatia kusimama kwa kazi kwa muda kwa wafanyakazi waliokuwa wakishiriki katika ujenzi wa MKICC, waliolalamikia kucheleweshewa mishahara yao na kutaka walipwe stahiki zao.

Hata hivyo, pamoja na kampuni kueleza kuwa tatizo limetatuliwa na malipo kuanza kufanyika, hali hiyo inaweka umuhimu wa kuhakikisha mifumo ya malipo inakuwa ya uhakika ili kulinda haki za wafanyakazi na kuepusha usumbufu unaoweza kuathiri utekelezaji wa mradi huo.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post