Na Joseph Ngilisho | SIMANJIRO
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa shule hiyo, Justin Nyari, aliyewataka wahitimu hao kutambua kuwa kuhitimu darasa la saba si mwisho wa elimu, bali ni mwanzo wa hatua nyingine inayohitaji uwajibikaji, bidii na kujituma zaidi.
Nyari alitoa wito huo kupitia taarifa yake iliyosomwa na mwalimu wa shule hiyo, Diana Akama, katika mahafali ya sita ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibuni.
“Leo ni siku ya furaha na fahari, lakini kumbukeni kuhitimu darasa la saba si mwisho wa elimu yenu, ni mwanzo wa sura mpya. Shule ya sekondari mtakutana na mazingira mapya, marafiki wapya na majukumu makubwa zaidi,” alisema Nyari.
Aliwataka wanafunzi hao kutanguliza elimu, kusikiliza ushauri wa wazazi na walimu wao, pamoja na kujenga tabia zitakazowasaidia kutimiza ndoto zao na kuwa watu wenye manufaa kwa familia na taifa.
Alisisitiza umuhimu wa kujiepusha na makundi mabaya, utoro, udanganyifu, matumizi ya pombe na dawa za kulevya, mahusiano yasiyofaa na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wao.
“Msikubali kushinikizwa na marafiki kutenda mambo mabaya kwa sababu tu wengine wanafanya hivyo. Jifunzeni kusema hapana kwa jambo linalopingana na maadili na malengo yenu,” alisisitiza.
Aipongeza Serikali
Katika hatua nyingine, Nyari aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na watangulizi wake, kwa juhudi za kupanua fursa za elimu nchini, ikiwamo elimu bila malipo na upatikanaji wa nafasi za kujiunga na shule za sekondari.
“Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na watangulizi wake kwa kupanua fursa za elimu. Tunamuomba Mungu azidi kumbariki Rais wetu, viongozi wetu na taifa letu ili amani, umoja na maendeleo viendelee kuwepo,” alisema.
Aliwatakia wahitimu hao mafanikio katika masomo yao ya sekondari na maisha yao ya baadaye, akiwataka waondoke shuleni hapo wakiwa na misingi ya nidhamu, shukrani, uadilifu na azma ya kufikia malengo yao.
“Mnapoondoka Glisten, nendeni na shukrani, nidhamu, uadilifu na azma. Kumbukeni shule yenu, walimu wenu na misingi mizuri mliyofundishwa. Tunatarajia kuwaona mkifanya vizuri na kuwa raia wawajibikaji, wenye heshima na wenye tija,” alisema.
Aidha, Nyari aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuiamini shule hiyo na kushirikiana nayo katika malezi na elimu ya watoto wao, huku akiwapongeza walimu na wafanyakazi kwa kujitoa na kuchangia ukuaji wa kitaaluma na kimaadili wa wanafunzi.
Alisema ushirikiano kati ya shule, wazazi na walezi ni muhimu katika kuwajenga watoto wenye maarifa, maadili mema na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Ends

إرسال تعليق