MWENYEKITI WA MTAA ADAIWA KUPIGANA NA MWANANCHI MSIBANI ARUSHA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWENYEKITI wa Mtaa wa Mureti, Kata ya Mureti jijini Arusha, Dominic Kivuyo, anadaiwa kuzichapa kavukavu na mwananchi wake waliokuwa msibani baada ya kutofautiana kuhusu namna ya kushughulikia mgogoro wa kifamilia unaohusu haki za mjane wa marehemu.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kuhusu tukio hilo, mwenyekiti huyo aliitwa kusaidia kutatua mgogoro uliodaiwa kuhusisha ndugu wa marehemu kutaka kumnyima mjane haki zake, hali iliyowafanya baadhi ya wananchi kuingilia kati kumtetea.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi hawakuridhishwa na namna alivyoshughulikia suala hilo, wakimtuhumu kuonekana kuunga mkono upande wa ndugu wa marehemu.
Inadaiwa kuwa mvutano uliongezeka baada ya mwananchi mmoja kumwambia mwenyekiti huyo kuwa hawampendi, kauli inayodaiwa kumkasirisha na kusababisha waanze kurushiana ngumi.
Video ya tukio hilo inayosambaa inaonyesha baadhi ya wananchi wakiingilia kati kujaribu kuwatenganisha wawili hao, huku tukio hilo likizua taharuki katika eneo la msiba.
Tukio hilo linaibua maswali kuhusu wajibu wa viongozi wa mitaa katika kusuluhisha migogoro ya kifamilia kwa haki, busara na utulivu, hususan pale ambapo haki na maslahi ya wajane yanapohusika.
Ends

إرسال تعليق