Ad
Breaking🔥

MISS BANTU YAPAMBA MOTO ARUSHA, USAJILI WAANZA KWA KISHINDO WENYE MIILI YAO MAMBO MOTO,WADHAMINI WAKARIBISHWA MSHINDI KUIBUKA NA GARI ZITO

MISS BANTU KUINUA UREMBO WA MWANAMKE WA KIAFRIKA, AJIRA KUNUFAISHA WANAWAKE

Usajili kuanza Novemba 10 Arusha, washiriki miaka 18 hadi 45, waandaaji waombwa kuunga mkono hamasa za AFCON

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SHINDANO la urembo wa asili wa mwanamke wa Kiafrika, Miss Bantu Tanzania, linatarajia kuanza usajili wa washiriki Novemba 10, mwaka huu, jijini Arusha, likilenga kuibua vipaji, kukuza utamaduni wa Kiafrika na kufungua fursa za ajira na kiuchumi kwa wanawake.

Shindano hilo, ambalo litafanyika kwa msimu wake wa kwanza, linawalenga wanawake wenye umri wa miaka 18 hadi 45, bila kuweka vigezo vya urefu au maumbo ya mwili vinavyozoeleka katika mashindano mengine ya urembo, bali kuzingatia uzuri wa asili, afya, uwezo na mchango wa mwanamke katika jamii.

Usajili wa washiriki unatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 10 katika viunga vya Makumbusho ya Azimio la Arusha, baada ya waandaaji kupata kibali cha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kinachowaruhusu kuendesha mashindano hayo kwa kipindi cha mwaka mmoja.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha,Leo OKTOBA 30,2026 mshirika mwenza wa Miss Bantu Tanzania, Jackline Kesi, alisema shindano hilo si la kuonyesha urembo pekee, bali ni jukwaa la kumtambua mwanamke wa Kiafrika, kumwezesha kiuchumi na kumpa nafasi ya kutumia uwezo wake kuleta mabadiliko katika jamii.

Alisema waandaaji tayari wameanza utekelezaji wa shughuli za shindano hilo baada ya kupata kibali, huku wakilenga kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kujikwamua kiuchumi na kujitegemea.

Kwa upande wake, mwalimu wa mamiss na wanamitindo, Lisa Steven maarufu Lislamod, alisema Miss Bantu inalenga kusherehekea mwili wa mwanamke wa Kiafrika kwa kuondoa mitazamo finyu inayohusisha urembo na urefu au maumbo fulani ya mwili.

Alisema mashindano hayo yatakuwa na fursa mbalimbali za ajira kwa washiriki, ikiwemo kupata mafunzo, kushirikishwa na kampuni na taasisi mbalimbali pamoja na kuwa mabalozi wa bidhaa na huduma (brand ambassadors).

Lisa alisema kupitia ushirikiano na wadau na wafadhili, washiriki watapata nafasi ya kutumia vipaji na umaarufu watakaoupata kujipatia kipato, huku wakijenga uwezo wa kujitegemea.

Alisisitiza kuwa umri wa miaka 18 hadi 45 umezingatiwa ili kutoa nafasi kwa wanawake wengi zaidi kushiriki, akieleza kuwa kigezo muhimu si mwonekano wa nje pekee, bali pia afya na uwezo wa mshiriki.

Katika hatua nyingine, Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Benson Maneno, aliyemwakilisha Mkuu wa Kitengo cha Sanaa na Utamaduni, alisema halmashauri imekabidhi kibali cha BASATA kwa taasisi ya Hibri Institute of Technology, kinachoiruhusu kuendesha mashindano hayo katika wigo wa kitaifa.

Maneno aliwapongeza waandaaji kwa kupata kibali hicho, akisema halmashauri inatambua mchango wa wadau wa sanaa na utamaduni katika kuendeleza vipaji na kuitangaza jamii kupitia shughuli za ubunifu.

Aidha, aliwataka waandaaji kuunganisha mashindano hayo na kampeni za kuhamasisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), akisema washiriki wanaweza kuwa sehemu ya kuitangaza Tanzania na kuhamasisha wananchi kushiriki katika tukio hilo kubwa la michezo.

Alisema matarajio ya halmashauri ni kuona washiriki wa Miss Bantu wakishiriki shughuli za hamasa kuelekea AFCON na kuwepo katika mechi ya ufunguzi itakayofanyika Uwanja wa Samia.

Alisema ushiriki wa wadau wa sanaa katika matukio makubwa ya kitaifa ni fursa ya kuonyesha utamaduni, vipaji na ubunifu wa Watanzania, huku ukiimarisha taswira ya nchi kimataifa.

Kwa ujumla, Miss Bantu Tanzania inatarajiwa kuwa jukwaa la kuunganisha urembo wa asili, utamaduni, uwezeshaji wa wanawake na fursa za kiuchumi, likilenga kuonyesha kuwa thamani ya mwanamke haipimwi kwa maumbo ya mwili pekee, bali pia uwezo, vipaji na mchango wake katika maendeleo ya jamii.







Ends

Post a Comment

أحدث أقدم