Ad
Breaking🔥

MAYUNGI: UKAGUZI WA MAZINGIRA ULINDE MUSTAKABALI WA DUNIA

 MAYUNGI: UKAGUZI WA MAZINGIRA ULINDE MUSTAKABALI WA DUNIA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Mayungi, amesema ukaguzi wa mazingira unapaswa kwenda zaidi ili kubaini matumizi ya fedha za umma na kulenga kulinda rasilimali za asili zinazotegemewa na mamilioni ya watu barani Afrika na duniani.

Alisema Afrika ina utajiri mkubwa wa misitu, madini, wanyamapori na vyanzo vya maji, hivyo udhaifu katika usimamizi wake unaweza kuathiri uchumi, afya za wananchi na maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Dkt. Mayungi alitoa kauli hiyo jijini Arusha OKTOBA 27,2026 alipofungua kwa niaba ya Naibu Waziri Mkutano Mkuu wa 12 wa Mwaka 2026 wa Kikundi Kazi cha Ukaguzi wa Mazingira cha Shirika la Taasisi za Juu za Ukaguzi wa Mazingira Barani Afrika (AFROSAI-WGE) ukijumuisha nchi 32.

Akizungumza katika mkutano huo, alisema ukaguzi wa mazingira una nafasi muhimu katika kuhakikisha sera na sheria za uhifadhi zinatekelezwa, fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya mazingira zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na serikali zinawajibika kwa matokeo ya hatua zinazochukua.

“Kwa kutafakari umuhimu wa kazi hii, nimejiuliza swali, tunakagua nini kama Afrika na kwa nini kazi hiyo ni muhimu? Jibu langu ni kwamba mnakagua mustakabali wa dunia. Hii si ukaguzi wa mazingira ya Afrika pekee, bali ni ukaguzi wa rasilimali zinazochangia maisha na uchumi wa dunia,” alisema.


Alisema kauli hiyo ina uzito kutokana na nafasi ya Afrika katika uhifadhi wa mifumo ya ikolojia duniani, uzalishaji wa malighafi za teknolojia za kisasa na usimamizi wa rasilimali za maji zinazotumiwa na nchi nyingi.

Alitaja Bonde la Kongo kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya misitu duniani, huku mito na maziwa makubwa, yakiwamo Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa, yakihitaji usimamizi endelevu ili kulinda upatikanaji wa maji na kupunguza athari za uchafuzi.

Alisema rasilimali hizo haziwezi kulindwa kwa ufanisi bila mifumo imara ya uwajibikaji, ukaguzi unaotegemea ushahidi na ushirikiano wa nchi zinazotegemeana katika matumizi ya rasilimali zinazovuka mipaka yake.

Akizungumzia hatua za Tanzania, Dkt. Mayungi alisema uhifadhi wa mazingira ni sehemu muhimu ya mkakati wa maendeleo ya taifa, kama inavyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia nguzo ya uadilifu wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.


Alisema nguzo hiyo inalenga kulinda bioanuwai, kusimamia matumizi endelevu ya maji na maeneo oevu, kudhibiti uchafuzi, kuimarisha matumizi bora ya ardhi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aliongeza kuwa serikali inaendeleza mipango ya matumizi ya ardhi, upangaji wa miji unaozingatia mazingira, usimamizi wa taka, uchumi wa mzunguko na matumizi ya nishati safi ili kuoanisha uhifadhi na ukuaji wa uchumi.

Alisema utekelezaji wa mipango hiyo unahitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha fedha na rasilimali zinazotengwa zinatoa matokeo yanayopimika kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere,ambaye ni Mwenyekiti wa Afrosal, alisema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano katika kusimamia rasilimali za maji kwa kuwa athari za maamuzi yanayofanywa katika nchi moja zinaweza kuonekana katika nchi nyingine.

Kichere, ambaye ni mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Ukaguzi wa Mazingira cha AFROSAI, alisema taasisi za ukaguzi zinapaswa kubadilishana taarifa na uzoefu ili kubaini changamoto za kimazingira zinazovuka mipaka ya kitaifa na kupendekeza hatua zinazoweza kutekelezwa kwa pamoja.

Alitoa mfano wa Ziwa Victoria na mfumo wa Mto Nile, akieleza kuwa rasilimali za maji zinazounganisha nchi mbalimbali zinahitaji usimamizi unaozingatia maslahi ya wananchi wote wanaozitegemea.

“Alisisitiza kuwa mipaka ya kisiasa haigawanyi athari za kimazingira zinazotokana na matumizi ya rasilimali zinazoshirikishwa na nchi mbalimbali"

Alisema taasisi za ukaguzi zina jukumu la kuchunguza iwapo ahadi za mazingira zinaingizwa katika mipango na bajeti za serikali, fedha za umma zinatumika ipasavyo na miradi inatekelezwa kwa kufikia malengo yaliyowekwa.

Aliongeza kuwa ripoti za ukaguzi zinapaswa kusaidia serikali kubaini mapungufu na kuchukua hatua za kurekebisha kasoro, huku teknolojia za kidijitali na mafunzo ya kitaalamu vikichangia kuongeza uwezo wa wakaguzi kutathmini taarifa za uendelevu.

Kichere alisema mafanikio ya ukaguzi wa mazingira hayapaswi kuishia katika kuandaa ripoti, bali yaonekane kupitia hatua zinazochukuliwa kulinda vyanzo vya maji, kudhibiti uchafuzi na kuhakikisha fedha za umma zinaleta manufaa yaliyokusudiwa.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za ukaguzi, serikali na mabunge, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuzingatia uhuru wa taasisi za ukaguzi katika kutekeleza majukumu yake.

Mkutano huo wa Arusha unajadili namna ukaguzi wa mazingira unavyoweza kuchangia uchumi wa kijani, usalama wa maji na udhibiti wa uchafuzi, huku ukilenga kuimarisha uwajibikaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za Afrika ili kufikia uchumi wa sh, trilion 1 mwaka 2050


Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post