Ad
Breaking🔥

DC SIMIYU AOKOA MWANAFUNZI KIDATO CHA NNE KUOZESHWA

DC SIMIYU AOKOA MWANAFUNZI KIDATO CHA NNE KUOZESHWA

…Aamuru sherehe ya kupokea mahari kusitishwa, wahusika kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi

Na Joseph Ngilisho | SIMIYU

MWANAFUNZI wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Igaganulwa, iliyopo Kata ya Dutwa, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, amenusurika kuozeshwa baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Simion Simalenga, akiongozana na askari, kuvamia eneo lililoandaliwa kwa ajili ya sherehe ya kupokea mahari yake.

Simalenga alifika nyumbani kwa dada wa mwanafunzi huyo na kukuta maandalizi ya sherehe yakiendelea, huku vyakula vikiwa vinaandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Baada ya kubaini kilichokuwa kikiendelea, mkuu huyo wa wilaya aliamuru shughuli zote kusimamishwa mara moja na watu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo kusambaa.

Katika hatua nyingine, Simalenga alimhoji mwanaume aliyekuwa akitarajiwa kumuoa mwanafunzi huyo, ambaye alifahamika kwa jina maarufu la Bonge, kuhusu uhusiano wake na binti huyo.

Hata hivyo, mwanaume huyo alidai kutomfahamu mwanafunzi huyo wala kutokujua jina lake, licha ya kuwa mahari yake ilikuwa ikipokelewa katika sherehe iliyokuwa ikiandaliwa.

Wahusika wa tukio hilo, akiwamo dada wa mwanafunzi huyo na mwanaume huyo, waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa hatua zaidi.

Jina la mwanafunzi huyo limehifadhiwa kwa sababu za kumlinda, huku tukio hilo likisisitiza umuhimu wa kulinda haki za watoto wa kike na kuhakikisha wanaendelea na masomo badala ya kuingizwa katika ndoa wakiwa bado shuleni.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post