Ad
Breaking🔥

LUKUMAY AIBANA SERIKALI UJENZI WA VITUO VYA AFYA KATIKA KATA TANO ARUMERU MAGHARIBI

LUKUMAY AITAKA SERIKALI KUJENGA VITUO VITANO VYA AFYA ARUMERU MAGHARIBI

Ahoji utekelezaji wa mpango wa kila kata kuwa na kituo cha afya, asema jimbo lina vituo nane pekee kati ya kata 27

Na Joseph Ngilisho | DODOMA

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, amehoji lini Serikali itajenga vituo vitano vya afya katika kata za Sambasha, Kimnyaki, Bangata, Musa na Kiranyi, akisema jimbo hilo lina vituo vya afya vinane pekee licha ya kuwa na kata 27.

Dkt Lukumay aliuliza swali hilo la nyongeza bungeni leo, akitaka Serikali kueleza mpango na muda wa utekelezaji wa ujenzi wa vituo hivyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila kata nchini inakuwa na kituo cha afya, hivyo akataka wananchi wa kata hizo tano za Arumeru Magharibi nao wanufaike na mpango huo.

“Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kwamba kila kata katika nchi hii ipate kituo cha afya. Jimbo la Arumeru Magharibi lina kata 27, lakini lina vituo nane tu vya afya,” alisema.

Alihoji: “Je, Serikali itajenga lini vituo vya afya vitano kwa miaka mitano kuanzia sasa katika kata za Sambasha, Kikimunyaku, Magata, Musa na Kiranyi?”

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya alisema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga vituo vya afya katika kila kata, lakini kwa sasa kipaumbele ni kata za kimkakati zenye idadi kubwa ya wananchi.

Alisema kuna baadhi ya kata ambazo mahitaji ya huduma yanaweza kutoshelezwa na zahanati, huku wananchi wakitumia vituo vya afya vilivyopo katika kata jirani.

Naibu Waziri aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wabunge na wananchi kuratibu mahitaji ya huduma za afya na utekelezaji wa ujenzi wa vituo hivyo.

Hata hivyo, katika majibu yake, Naibu Waziri hakutaja muda maalumu wa kuanza ujenzi wa vituo vitano vilivyopendekezwa na Dkt Lukumay.

Post a Comment

Previous Post Next Post