Ad
Breaking🔥

WEZI WA TOYO WAUAWA KWA RISASI NA POLISI ARUSHA,WALIWAHI KUFUNGWA WAKATOKA

YUZO NA NDESAA WAFARIKI BAADA YA MAPAMBANO NA POLISI ARUSHA

Watuhumiwa wa mauaji ya madereva bodaboda, uporaji wa pikipiki wakutwa na bastola, panga

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Watuhumiwa wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya mauaji na uporaji wa pikipiki jijini Arusha na maeneo jirani, wamefariki dunia baada ya kujeruhiwa katika mapambano na polisi eneo la Kijenge, jijini humo.

Watuhumiwa hao waliotajwa kwa majina ya Yusuph Hamis maarufu Yuzo na Dickson Livingstone, anayefahamika kwa jina la Ndesaa, walifariki dunia wakiwa hospitalini walikokuwa wakipatiwa matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata katika tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 21, 2026, saa 3:30 usiku, wakati askari walipowadhibiti watuhumiwa hao waliokuwa wakijiandaa kutekeleza tukio jingine la uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 22, 2026, Masejo alisema watuhumiwa hao walijeruhiwa wakati wakijaribu kujihami kwa silaha ili kuzuia kukamatwa.

Alisema polisi waliwakamata katika mazingira ya mapambano, huku wakiwa na bastola na panga ambazo zinadaiwa kutumiwa kujihami wakati wa shughuli zao za kihalifu.

Aidha, alisema walikutwa na pikipiki mpya isiyokuwa na namba za usajili, hali iliyozua shaka kuhusu utambulisho wake na chanzo chake.

WAHUSISHWA NA MAUAJI YA BODABODA

Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, Yuzo alikuwa akituhumiwa kuongoza genge la uhalifu linalodaiwa kuhusika na matukio mbalimbali, yakiwemo mauaji ya madereva bodaboda na uporaji wa pikipiki zao.

Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya Erasto Losujaki, dereva bodaboda na mkazi wa Kisongo, ambaye mwili wake ulikutwa kando ya barabara katika kitongoji cha Olkaria, Kata ya Mateves, Wilaya ya Arumeru, Aprili 28, 2026, huku pikipiki yake ikiwa imeporwa.

Tukio jingine ni mauaji ya Adiel Thomas Spitari, dereva bodaboda na mkazi wa Ngaramtoni, ambaye aliuawa Septemba 15, 2026, katika Kijiji cha Likamba, Kata ya Musa, Wilaya ya Arumeru, baada ya kudaiwa kuporwa pikipiki yake.

Kamanda Masejo alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini kwa kina uhusiano wa watuhumiwa hao na matukio hayo pamoja na makosa mengine wanayotuhumiwa kuyatenda.

WALIWAHI KUFUNGWA

Masejo alisema watuhumiwa hao waliwahi kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa makosa mbalimbali, yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, kuvunja nyumba na wizi.

Aliongeza kuwa Ndesaa alikuwa bado akitumikia kifungo cha nje wakati wa tukio hilo.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea kuwafuatilia watu wengine wanaodaiwa kushirikiana na watuhumiwa hao katika matukio ya uhalifu, pamoja na kufuatilia mali zinazodaiwa kuporwa, zikiwemo pikipiki.

Polisi limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na watu wanaotiliwa shaka ili kusaidia kuimarisha usalama wa raia na mali zao.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post