Ad
Breaking🔥

LUGANGIRA AKUTANA NA UPINZANI, ASISITIZA MARIDHIANO ARUMERU


LUGANGIRA AKUTANA NA UPINZANI, ASISITIZA MARIDHIANO ARUMERU

Atoa wito wa ushirikiano kuvuka tofauti za kisiasa, CHADEMA na UPDP waunga mkono hatua hiyo

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amekutana na wawakilishi wa vyama vya upinzani wilayani humo na kusisitiza umuhimu wa maridhiano, mawasiliano na ushirikiano kati ya Serikali na vyama vya siasa ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Lugangira ametoa msisitizo huo katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake, ikiwa ni sehemu ya hatua zake za awali za kufahamu wilaya na wadau wake, huku akieleza kuwa tofauti za kiitikadi hazipaswi kuwa kikwazo katika kutatua changamoto za wananchi na kuboresha huduma za kijamii.

Amesema dhamira yake ni kushirikiana na wadau wote bila kujali itikadi za kisiasa, kwa kuzingatia misingi ya 4R iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayojumuisha maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kudumisha amani, kuimarisha mshikamano na kuhakikisha wananchi wa Arumeru wananufaika na huduma bora pamoja na fursa za maendeleo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo ya Rais unahitaji ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.

Akizungumza katika mazungumzo hayo, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa Arumeru Mashariki, Pallangyo Penzila, amempongeza Lugangira kwa kuanza majukumu yake kwa kujifunza na kuifahamu wilaya pamoja na wananchi wake.

Penzila amesema kuifahamu jamii na mazingira ya eneo husika ni msingi muhimu kwa kiongozi anayekabidhiwa majukumu mapya, kwa kuwa humsaidia kufanya maamuzi yanayozingatia mahitaji halisi ya wananchi.

Ameeleza kuwa elimu na uzoefu wa Lugangira katika utumishi wa umma vinaweza kusaidia kuchochea maendeleo ya wananchi wa Meru, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na vyama vya siasa bila kujali tofauti zao za kiitikadi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP) wa Arumeru Mashariki, Magdalena Masaka, amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuanza majukumu yake kwa kukutana na wawakilishi wa vyama vya siasa.

Masaka amesema hatua hiyo inaonesha nafasi ya mazungumzo katika kujenga uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa kisiasa, akibainisha kuwa wajibu wa vyama vya siasa hauishii katika kushiriki uchaguzi, bali pia unahusisha kushiriki katika juhudi za kuleta maendeleo, kulinda amani na kudumisha utulivu.

Amesema vyama vya upinzani viko tayari kushirikiana na Mkuu wa Wilaya pamoja na Serikali kwa ujumla katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi na kuhakikisha juhudi za maendeleo zinawanufaisha wakazi wa Arumeru.

Mazungumzo hayo yanaweka msisitizo katika umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa, kwa lengo la kujenga mazingira ya ushirikiano katika kushughulikia masuala yanayogusa maisha ya wananchi.


Ends

Post a Comment

أحدث أقدم