KWEKA ADAIWA KUMUUA MKE KWA RISASI, AJISALIMISHA POLISI
• Wivu wa mapenzi watajwa kuwa chanzo cha tukio
Na ArushaDigital| DAR ES SALAAM
MKAZI wa Bunju A jijini Dar es Salaam, anayetajwa kwa jina la Laurent Kweka, anadaiwa kumpiga risasi na kumuua mke wake, Jenipher, ndani ya nyumba yao iliyopo Mtaa wa Mkoani, eneo la Senzele.
Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea katika majira ya alfajiri ya Oktoba 1, 2026, huku taarifa za awali zikidai kuwa wivu wa mapenzi unaweza kuwa chanzo cha tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na Millard Ayo, Mwenyekiti wa Shina la Mtaa wa Mkoani, Lucia Shirima, amesema taarifa za tukio hilo zilifika kwa viongozi baada ya mfanyakazi wa ndani wa familia hiyo kutoa taarifa akisema, “Baba amemuua Mama.”
Shirima amesema baada ya kupata taarifa hiyo, alifika katika eneo la tukio na kuwasiliana na viongozi pamoja na Jeshi la Polisi.
Walipofika nyumbani hapo, walidaiwa kuukuta mwili wa Jenipher ukiwa pembeni ya kitanda.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati viongozi na polisi walipofika eneo la tukio, Kweka hakuwepo, huku baadaye ikielezwa kuwa alikuwa amekwenda katika kituo cha polisi na kujisalimu mwenyewe.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi iliyotolewa hadharani kuthibitisha chanzo cha tukio hilo, mazingira ya mauaji hayo au hatua zilizochukuliwa dhidi ya Kweka.
Taarifa zaidi zinatarajiwa kutoka kwa Jeshi la Polisi ili kuweka wazi mazingira ya tukio hilo na hatua za kisheria zinazochukuliwa.
Ends

إرسال تعليق