KAMATI YA BUNGE YATOA MAAGIZO MAZITO BARABARA ZA AFCON ARUSHA
...Yataka kilometa 13 zikamilike kwa wakati, vifaa viongezwe na wafanyakazi walipwe stahiki zao
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imewataka wakandarasi wanaojenga barabara za maandalizi ya AFCON jijini Arusha kuongeza kasi ya ujenzi, kuongeza vifaa katika maeneo yenye ucheleweshaji na kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa stahiki zao kwa wakati, bila kuathiri ubora wa kazi.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abubakari Asenga, alisema Oktoba 24, 2026, baada ya kamati kukagua miradi ya barabara mkoani Arusha, kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzania kuandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Alisema Serikali imeingia mikataba ya ujenzi wa takribani kilometa 70 za barabara, huku kilometa 13 zikiwa miongoni mwa zinazohitaji kukamilishwa kwa haraka kutokana na umuhimu wake katika kuunganisha Jiji la Arusha na maeneo ya michezo.
Asenga alisema miradi hiyo ina thamani inayokadiriwa kufikia Sh bilioni 54, akisisitiza kuwa kamati itaendelea kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa.
“Tunawahi AFCON, lakini barabara hizi zitabaki baada ya AFCON. Hatuwezi kujenga kwa haraka leo halafu baadaye tukazirudia kwa sababu ya kutokuzingatia ubora. Tunataka zikamilike kwa wakati, lakini kwa viwango vinavyotakiwa,” alisema.
Alisema kamati imeagiza miradi inayoonekana kuwa na changamoto za utekelezaji, ikiwemo barabara ya mzunguko ya Mbouda, kuongezewa mitambo ya kuchimba, magreda na malori ili kuongeza kasi ya kazi na kuzuia ucheleweshaji zaidi.
Aidha, alisema mamlaka za Serikali za wilaya na wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi wanaoathiriwa na ujenzi huo, hususan kuhusu changamoto zinazohusiana na maji, umeme na nyaya zinazopita juu ya nyumba.
Alisema maendeleo ya miundombinu yanapaswa kwenda sambamba na ushirikiano wa mamlaka husika katika kutatua kero za wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotekelezewa miradi hiyo.
Katika hatua nyingine, Asenga alisema kamati imesisitiza umuhimu wa kuwalipa kwa wakati vibarua na wafanyakazi wanaotekeleza miradi hiyo, pamoja na kuhakikisha michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii na stahiki nyingine zinawasilishwa kwa wakati.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza morali ya wafanyakazi na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa bidii, ikiwemo kufanya kazi usiku na mchana pale inapohitajika.
Asenga alisema kamati inatambua juhudi zinazofanywa na Serikali, viongozi wa mkoa na wilaya pamoja na wabunge katika kusimamia maandalizi ya AFCON, huku akiwataka wahandisi washauri, wakandarasi na wataalamu kuhakikisha kazi zinafanyika kwa mujibu wa mikataba na viwango vilivyokubaliwa.
Alisema kamati inatarajia kurejea Arusha Januari 2027 kukagua maendeleo ya miradi hiyo na kuendelea na ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha maelekezo ya Serikali kuhusu maandalizi ya AFCON yanatekelezwa.
Alisisitiza kuwa Tanzania inapaswa kutumia maandalizi ya michuano hiyo kujenga miundombinu imara itakayodumu kwa miaka mingi, badala ya kuzingatia mahitaji ya mashindano pekee.
“Wataalamu wetu mna jukumu kubwa. Fanyeni kazi kwa mujibu wa mikataba, viwango na maslahi ya nchi yetu. Tanzania inawategemea kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa ubora unaostahili,” alisema.
WIZARA YAPOKEA MAAGIZO
Akizungumza baada ya kamati hiyo kukagua miradi hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema wizara imepokea maelekezo yaliyotolewa na kamati na itayafanyia kazi ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.
Alisema Serikali haitamwangusha Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa barabara zinazojengwa zitakuwa na njia nne, njia za watembea kwa miguu na taa za barabarani.
Alisema miundombinu hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa magari, kurahisisha usafiri wa wachezaji na mashabiki wa soka wakati wa AFCON na kuboresha mandhari ya Jiji la Arusha.
Aidha, Kasekenya alisema Serikali inaendelea kuboresha sehemu zilizochakaa za barabara kutoka Arusha hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ili kuhakikisha wageni watakaokuja nchini kwa ajili ya michuano hiyo wanakutana na miundombinu yenye viwango vinavyostahili.
Ends

إرسال تعليق