Ad
Breaking🔥

JITIHADA ZA MBUNGE LUKUMAY ZALETA MAPINDUZI SEKTA YA AFYA ARUMERU, WABUNGE IPU WATUA JIMBONI WAJENGA ZAHANATI,AMSHUKURU RAIS SAMIA.

JITIHADA ZA MBUNGE LUKUMAY ZALETA MABADILIKO ARUMERU WABUNGE IPU  WATUA JIMBONI WAJENGA ZAHANATI,AMSHUKURU RAIS SAMIA.

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lembulung Lukumay, amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo umeendelea kuimarisha huduma za afya ya msingi nchini, akisema ziara za wabunge wanaoshiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika miradi ya maendeleo zinaweza kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.


Lukumay, ambaye pia ni daktari wa binadamu, amesema hayo Oktoba 6,2026 wakati Kamati ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa ndani ya IPU ilipotembelea Zahanati ya Kioga, Ilkiding’a, Jimbo la Arumeru Magharibi, kujionea huduma zinazotolewa pamoja na jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD) lililojengwa kwa msaada wa Sh milioni 264 kutoka Benki ya Dunia.

Amesema ziara hiyo imeonyesha namna ushirikiano wa kimataifa unavyoweza kusaidia Serikali kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.

“Tunawashukuru wadau wetu ambao wameendelea kushirikiana nasi. Benki ya Dunia imesaidia ujenzi wa jengo hili la OPD, wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likisaidia katika maeneo mbalimbali kuhakikisha huduma zinatolewa, watoto wanasajiliwa, dawa zinapatikana na watumishi wanapata elimu,” amesema.

Amesema UNICEF nayo imeendelea kusaidia katika utoaji wa chanjo, ikiwamo chanjo za polio na kampeni nyingine za afya.





Lukumay amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele katika afya ya msingi na kuweka mazingira yanayowawezesha wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana na Serikali kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema Serikali imejenga vituo vya afya 649 na zahanati 2,700 nchini, huku Zahanati ya Kioga ikiwa miongoni mwa vituo vinavyotoa huduma kwa wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi.

“Ukienda hapa unaona maabara, vifaa vya tiba na dawa zinapatikana. Serikali inaendelea kutoa fedha kuhakikisha dawa zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi,” amesema.

Kwa mujibu wa Lukumay, Serikali imeendelea pia kuwekeza katika ngazi nyingine za huduma za afya, ikiwamo ujenzi wa hospitali 119 za wilaya na uboreshaji wa hospitali za mikoa na za rufaa kwa kupeleka vifaa vya kisasa.

Hata hivyo, amesema pamoja na hatua hizo, changamoto katika sekta ya afya bado ni kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kuboreshwa.

“Changamoto bado ni kubwa, hasa katika sekta ya afya. Serikali imefanya mambo makubwa katika afya, lakini tunahitaji ushirikiano wa wananchi na wadau ili kuhakikisha huduma zinaendelea kuwa bora,” amesema.

Amesema Tanzania inapaswa kutumia fursa za mikutano ya kimataifa kama IPU kuwaonyesha wageni miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini na mahitaji yaliyopo, ili kuwavutia wadau zaidi kushiriki katika kuimarisha huduma za kijamii.

Lukumay pia amewashukuru wananchi wa Ilkiding’a na Jimbo la Arumeru Magharibi kwa mapokezi waliyowapa wageni hao, akiwataka kuendelea kushirikiana na Serikali na kuwakaribisha wadau wanaokuja nchini kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo.

Amesema kudumisha amani ni jambo la msingi katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa na kuwanufaisha wananchi.

“Tanzania haina nchi nyingine. Tukidumisha amani, maendeleo yataendelea kuonekana kwa wananchi wetu,” amesema.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post