Ad
Breaking🔥

BALOZI HOYCE TEMU AAHIDI KUTUMIA FURSA ZA IPU NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA KULETA MAENDELEO NCHINI

TEMU: TUTUMIE FURSA ZA IPU KUVUTIA MIRADI YA MAENDELEO

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU


BALOZI na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa yaliyopo Geneva, Uswisi, Hoyce Temu, amesema Tanzania inapaswa kutumia fursa zinazopatikana kupitia jumuiya ya kimataifa kuwashawishi wadau na mashirika mbalimbali duniani kuunga mkono miradi ya maendeleo nchini.

Temu amesema hayo Oktoba 6,2026  wakati wa ziara ya Kamati ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa ndani ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) iliyotembelea zahanati ya Kijiji Cha Kioga wilayani Arumeru kujionea mradi wa zahanati uliojengwa kwa fedha kutoka IPU huku ikiwa ni sehemu ya jitihada za mbunge wa Arumeru Magharibi dkt Johannes Lukumay kuhakikisha Jimbo hilo linakuwa na zahanati za kutosha.

 Amesema ziara hiyo ni sehemu ya fursa zinazotokana na kufanyika kwa Mkutano wa 153 wa IPU jijini Arusha, unaowakutanisha wabunge na viongozi wa mabunge kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Temu, uwepo wa wawakilishi hao nchini unatoa nafasi kwa Tanzania kuwaonyesha moja kwa moja miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na taasisi za kimataifa, hatua ambayo inaweza kusaidia kuvutia misaada, uwekezaji na miradi mipya ya maendeleo.

Amesema Tanzania kupitia uwakilishi wake Geneva inaendelea kufuatilia fursa zinazopatikana katika mashirika mbalimbali ya kimataifa na kuzitumia kwa manufaa ya nchi.

“Wajibu wetu ni kuangalia fursa mbalimbali duniani kupitia mashirika ya kimataifa yaliyopo Geneva, New York na maeneo mengine, kuhakikisha Tanzania inapata fursa na inakuwa mwanachama hai. Tunapaswa kutumia fursa hizo kuleta maendeleo,” amesema.

Amesema mradi wa zahanati walioutembelea ni mfano wa namna ushirikiano wa kimataifa unavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa lengo ni kuona miradi ya aina hiyo ikiendelea kuongezeka katika maeneo mengine.

Temu amesema Kamati hiyo baada ya kujionea mradi huo itafanya tathmini na kuangalia maeneo mengine ambayo yanaweza kupewa kipaumbele katika ushirikiano wa maendeleo.

Amesema Tanzania inapaswa kutumia nafasi yake katika IPU na mashirika mengine ya kimataifa kuimarisha ushirikiano na kupata fursa zaidi za maendeleo.

Ameongeza kuwa kufanyika kwa Mkutano wa 153 wa IPU jijini Arusha ni fursa muhimu kwa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla, kwa kuwa umeleta nchini maelfu ya wajumbe kutoka mabunge mbalimbali duniani.

“Tunataka fursa zinazotokana na mkutano huu zirejee kwa wananchi, hasa jamii ya Arusha ambako mkutano huu umefanyika,” amesema.









Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post