DC TAMBO AWAONYA WAKANDARASI WANAOCHELEWESHA MIRADI
...Aanza ukaguzi wa miradi Arusha, ataja Oktoba 18 na 19
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Nicodemas Tambo, ameonya wakandarasi wanaolipwa fedha za Serikali bila kukamilisha miradi kwa wakati, akisema ataanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ili kubaini changamoto na kuwawajibisha wanaoshindwa kutekeleza mikataba yao.
Alisema moja ya maelekezo aliyoyapokea kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha miradi yote iliyoanzishwa na Serikali inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
“Nimepata taarifa kuwa kuna wakandarasi ambao wamelipwa fedha za Serikali lakini hawajamaliza miradi yao. Nitaenda kukagua miradi hiyo ili kujua sababu za kutokamilika kwake,” alisema Tambo.
Alisema anatarajia kuanza ziara hiyo Oktoba 18 na 19, mwaka huu, kwa kutembelea miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ili kujiridhisha na hatua iliyofikiwa na kubaini sababu za ucheleweshaji.
Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wakandarasi waliokamilisha miradi waliyopewa, akiwataka viongozi na wataalamu wa Serikali kuendelea kushirikiana na wakandarasi wenye dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Barabara kuongeza thamani ya maeneo
Akizungumzia manufaa ya barabara hiyo, Tambo alisema ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami una mchango katika kurahisisha usafiri, kukuza biashara na kuongeza thamani ya maeneo yanayozunguka miundombinu hiyo.
Alisema barabara bora zinawarahisishia wananchi kusafirisha bidhaa, kufika sokoni na maeneo ya kazi, huku zikiwapa wafanyabiashara fursa ya kupanua shughuli zao.
Aliongeza kuwa miundombinu inayoboreshwa inaweza kuongeza thamani ya majengo na maeneo ya biashara, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hizo kukuza uchumi wao.
Tambo aliwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, wakiwamo meya na madiwani, kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema atasimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa kushirikiana na viongozi wengine ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ataka Arusha kunufaika na AFCON
Katika hatua nyingine, Tambo aliwataka wakazi wa Arusha na wafanyabiashara kujiandaa kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Alisema uwekezaji unaofanywa katika miundombinu na maandalizi ya mashindano hayo unapaswa kuambatana na mikakati ya wananchi kunufaika kupitia biashara, huduma za malazi, migahawa, usafiri na utalii.
“Wageni watakapokuja Arusha, watalala kwenye hoteli zetu, watanunua chakula, watatumia huduma mbalimbali na kutembelea hifadhi za wanyamapori. Hizo zote ni fursa za fedha kwa wananchi wetu,” alisema.
Aliwataka wafanyabiashara kuboresha huduma zao na kujiandaa kupokea wageni, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha fursa zitakazotokana na mashindano hayo zinachangia kukuza uchumi wa jiji na kuongeza kipato cha wananchi.
Tambo alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo, hivyo ni muhimu wananchi, viongozi na wafanyabiashara kushirikiana kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yanayoonekana.
Ends..




إرسال تعليق