Ad
Breaking🔥

DC LUGANGIRA ASHUHUDIA MAKABIDHIANO YA EKARI 23 KWA JAMII YA MAASAI,AHIMIZA LITUMIKE PIA KUHAMASISHA ELIMU KWA MTOTO WA KIKE

EKARI 23 ZA WAMAASAI ZITUMIKE KUKOMESHA NDOA ZA UTOTONI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SERIKALI imewataka viongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai kuhakikisha eneo la ekari 23 lililokabidhiwa kwa jamii hiyo na Kampuni ya Burka Coffee Estate linatumika kuendeleza mila na desturi zinazolinda ustawi wa jamii, huku likiwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike na kupambana na ndoa za utotoni.

Serikali imesema upatikanaji wa eneo hilo unapaswa kuwa fursa ya kuimarisha maendeleo ya jamii, ikiwataka viongozi wa kimila kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wa kike hawanyimwi haki ya kupata elimu kwa kisingizio cha mila na desturi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, katika hafla ya makubaliano na makabidhiano ya eneo hilo lililokuwa na hati ya umiliki wa Kampuni ya Burka Coffee Estate baada ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 kutatuliwa.

Akizungumza katika hafla hiyo oktoba 16,2026, Lugangira alisema Serikali inatambua umuhimu wa kutatua migogoro kwa mazungumzo, haki na kuheshimiana, lakini akasisitiza kuwa mafanikio ya maridhiano hayo yanapaswa kuonekana pia katika hatua za kuboresha maisha ya jamii husika.

Alisema viongozi wa kimila wana nafasi kubwa ya kutumia eneo hilo kuimarisha utamaduni wa Kimaasai sambamba na kuhamasisha mabadiliko chanya yatakayowawezesha watoto kupata haki zao za msingi, hususan elimu.

“Nimefurahi kusikia kwamba katika baraza lenu mnasimamia masuala ya kuhakikisha watoto wanaenda shule. Naomba tushirikiane kuhakikisha watoto wa kike hawanyimwi haki yao ya msingi ya kupata elimu, lakini muhimu zaidi tushirikiane kupambana na kutokomeza changamoto ya ndoa za utotoni,” alisema Lugangira.

Alisema jamii inapaswa kutambua kuwa elimu ni msingi muhimu wa maendeleo, hivyo ni wajibu wa viongozi wa kimila, wazazi na Serikali kuweka mazingira yanayowawezesha watoto wa kike kuendelea na masomo badala ya kuingia katika ndoa wakiwa bado na umri mdogo.



Lugangira alieleza kuwa jamii inahitaji wanawake wengi waliosoma na kushiriki katika uongozi na maendeleo, akitolea mfano wanawake waliofanikiwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kuwa ushahidi wa umuhimu wa kumpa mtoto wa kike fursa ya elimu.

Aliahidi kuwa Serikali ya Wilaya ya Arumeru itaendelea kushirikiana na viongozi wa kimila katika kuweka mazingira wezeshi kwa watoto wa kike kupata elimu na kupunguza changamoto ya ndoa za utotoni.

Atoa wito wa kuendeleza utalii wa utamaduni

Katika hatua nyingine, Lugangira aliwataka viongozi wa kimila kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Arusha kuendeleza utalii wa utamaduni, akisema upanuzi wa shughuli za utalii na maendeleo katika Jiji la Arusha unaongeza umuhimu wa kutumia fursa zilizopo katika Wilaya ya Arumeru.

Alisema eneo hilo linaweza kuwa sehemu ya kuhifadhi na kuendeleza mila, desturi na historia ya jamii ya Kimaasai, huku likichangia kukuza utalii na uchumi wa wananchi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa juhudi za kuhifadhi utamaduni zinapaswa kwenda sambamba na kulinda haki za watoto na kuhakikisha mila hazitumiki kama kikwazo cha elimu kwa mtoto wa kike.

Mgogoro wa zaidi ya miaka 10 watatuliwa

Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 23 limekabidhiwa kwa jamii ya Kimaasai kupitia Baraza Kuu la Viongozi wa Kimila wa Kimaasai Tanzania (MARYA), baada ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 kati ya jamii hiyo na Kampuni ya Burka Coffee Estate kufikia maridhiano.

Kampuni hiyo ilikuwa na hati ya umiliki wa eneo hilo kabla ya makubaliano yaliyofanikisha kumalizika kwa mgogoro na kukabidhiwa kwa jamii kwa ajili ya shughuli za kimila.

Lugangira aliwataka wahusika wote kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na kukamilisha taratibu za kisheria zinazohitajika, akisisitiza kuwa Serikali haitarajii kuona utekelezaji wake ukikwama au kusuasua.

Alisema utatuzi wa mgogoro huo unapaswa kuwa mwanzo wa ushirikiano endelevu kati ya jamii na kampuni, huku manufaa ya makubaliano yakichangia ustawi wa jamii na maendeleo ya eneo hilo.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم