LISSU AFIKA FAINALI YA TUZO YA SAKHAROV, ICC YASHINDA
By Arushadigital
KIONGOZI wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, amefika hatua ya fainali ya Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Fikra ya mwaka 2026, huku Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na maafisa wake wakitangazwa washindi wa tuzo hiyo inayotolewa na Bunge la Ulaya.Rais wa Bunge hilo, Roberta Metsola, alitangaza mshindi Oktoba 22, 2026, jijini Strasbourg, Ufaransa, katika tuzo inayotambua mchango wa watu binafsi na taasisi katika kutetea haki za binadamu, demokrasia na uhuru wa msingi.
Lissu, ambaye amekuwa akipigania demokrasia na uchaguzi huru na wa haki nchini Tanzania, alikuwa miongoni mwa waliowania tuzo hiyo hadi hatua ya mwisho, akitambuliwa kutokana na juhudi zake katika kutetea misingi ya utawala wa kidemokrasia.
Kufika kwake fainali kunakuja wakati Tanzania ikiendelea kukabiliwa na mijadala kuhusu hali ya demokrasia, uhuru wa kisiasa na mazingira ya utendaji wa vyama vya upinzani.
Kwa upande wake, ICC na maafisa wake wametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wao katika kuendeleza uwajibikaji kwa uhalifu mkubwa wa kimataifa na kusimamia utawala wa sheria.
Uamuzi huo umetolewa wakati mahakama hiyo ikikabiliwa na shinikizo la kisiasa na kidiplomasia, likiwamo hatua za Marekani kuweka vikwazo dhidi ya baadhi ya maafisa wake kutokana na shughuli za mahakama hiyo katika kesi nyeti za kimataifa.
Tuzo ya Sakharov, iliyopewa jina la mwanasayansi na mwanaharakati wa haki za binadamu wa zamani wa Umoja wa Kisovieti, Andrei Sakharov, hutolewa kila mwaka na Bunge la Ulaya kwa watu au taasisi zinazochangia kwa kiwango kikubwa kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi.
Sherehe za kukabidhi tuzo hiyo zimepangwa kufanyika Desemba 16, 2026, jijini Strasbourg, Ufaransa.
Ends
Post a Comment