KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA MIRADI YA AFCON ARUSHA
Yataka kilometa 13 zikamilike kwa wakati, vifaa viongezwe na wafanyakazi walipwe stahiki zao
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepongeza juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya barabara za maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) jijini Arusha, huku ikitoa maagizo kwa wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi, vifaa na kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa stahiki zao kwa wakati.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abubakari Asenga, alisema Oktoba 24, 2026, baada ya kukagua miradi hiyo kuwa, pamoja na pongezi hizo, kamati inataka wakandarasi kuhakikisha barabara hizo zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, bila kuathiri ubora wa miundombinu itakayotumika hata baada ya mashindano hayo.
Alisema Serikali imeingia mikataba ya ujenzi wa takribani kilometa 70 za barabara, huku kilometa 13 zikitajwa kuwa sehemu inayohitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake katika maandalizi ya AFCON.
Asenga alisema miradi hiyo ina thamani inayokadiriwa kufikia Sh bilioni 54, akisisitiza kuwa kamati itaendelea kuisimamia ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo na kazi zinafanyika kwa mujibu wa mikataba.
Alisema kamati imeelekeza miradi yenye changamoto za utekelezaji, ikiwemo barabara ya mzunguko ya Mbouda, kuongezewa mitambo ya kuchimba, magreda na malori ili kuongeza kasi ya kazi na kuzuia ucheleweshaji zaidi.
Aidha, aliwataka wakandarasi na wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kushirikiana na viongozi wa Serikali za wilaya kutoa elimu kwa wananchi wanaoathiriwa na ujenzi, hususan kuhusu changamoto za huduma za maji, umeme na nyaya zinazopita juu ya nyumba.
Alisema maendeleo ya miundombinu yanapaswa kwenda sambamba na utatuzi wa kero za wananchi, akisisitiza kuwa mamlaka zinazohusika zinapaswa kushirikiana kwa karibu kuhakikisha changamoto hizo hazikwamishi utekelezaji wa miradi wala kuwaongezea wananchi usumbufu usio wa lazima.
Katika hatua nyingine, Asenga alisisitiza umuhimu wa kuwalipa kwa wakati vibarua na wafanyakazi wanaotekeleza miradi hiyo, pamoja na kuwasilisha michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii na stahiki nyingine kwa mujibu wa taratibu.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza morali ya wafanyakazi na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ikiwemo kufanya kazi usiku na mchana pale inapohitajika ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Asenga alizipongeza Serikali, viongozi wa mkoa na wilaya pamoja na wabunge kwa juhudi za kusimamia maandalizi ya AFCON, huku akiwataka wahandisi washauri, wakandarasi na wataalamu kuzingatia mikataba, muda wa utekelezaji na viwango vya ubora vilivyokubaliwa.
Alisema kamati inatarajia kurejea Arusha Januari 2027 kukagua maendeleo ya miradi hiyo, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa yanatekelezwa.
Alisisitiza kuwa maandalizi ya AFCON yanapaswa kuwa fursa ya kuijengea Tanzania miundombinu imara na ya kudumu, badala ya kuangalia mahitaji ya mashindano pekee.
“Wataalamu wetu mna jukumu kubwa. Fanyeni kazi kwa mujibu wa mikataba, viwango na maslahi ya nchi yetu. Tanzania inawategemea kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa ubora unaostahili,” alisema.
WIZARA YAPOKEA MAAGIZO
Akizungumza baada ya kamati hiyo kukagua miradi hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema wizara imepokea maelekezo yaliyotolewa na kamati na itayafanyia kazi ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati.Alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu ya usafiri na kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kuandaa michuano hiyo ya kimataifa.
Kasekenya alisema barabara zinazojengwa zitakuwa na njia nne, njia za watembea kwa miguu pamoja na taa za barabarani, hatua inayolenga kurahisisha usafiri, kupunguza msongamano wa magari na kuboresha mandhari ya Jiji la Arusha.
Aliongeza kuwa miundombinu hiyo itakuwa na manufaa kwa wakazi wa Arusha na watumiaji wengine wa barabara hata baada ya kumalizika kwa AFCON, huku ikirahisisha usafiri wa wachezaji, viongozi na mashabiki watakaohudhuria mashindano hayo.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kuboresha sehemu zilizochakaa za barabara kutoka Arusha hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ili kuhakikisha wageni watakaotembelea Tanzania kwa ajili ya AFCON wanakutana na miundombinu inayokidhi viwango vinavyostahili.
Alisema wizara itaendelea kushirikiana na wakandarasi, wahandisi na mamlaka nyingine kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo zinatatuliwa kwa wakati, ili maandalizi ya AFCON yaendelee bila vikwazo visivyo vya lazima.
Ends










Post a Comment