Ad
Breaking🔥

WATU SITA AKIWEMO ASKARI WAUAWA KATIKA VURUGU HIFADHI YA ISWAGALA

WATU SITA WAAUAWA KATIKA VURUGU HIFADHI YA ISWAGALA

Na Joseph Ngilisho, Tabora

JESHI la Polisi Mkoa wa Tabora limeanza uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa watu sita, wakiwemo askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Walinzi wa Hifadhi za Vijiji (VGS) na madereva wawili, baada ya kundi la watu kuvamia kambi ya askari wa doria katika Hifadhi ya Wanyamapori Iswagala, iliyopo Kijiji cha Utimle, Wilaya ya Sikonge.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Twaha Lulengelule, amesema tukio hilo limetokea wakati askari hao walipokuwa wakishirikiana na maafisa wengine wa Halmashauri katika operesheni ya kukamata mifugo iliyodaiwa kuingizwa kinyume cha sheria ndani ya hifadhi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jioni hii, Kamanda Lulengelule amesema kundi la wafugaji lilivamia kambi hiyo likiwa na silaha za jadi na kuwashambulia askari pamoja na watu wengine waliokuwa katika eneo hilo.

Amesema katika vurugu hizo, watu sita walipoteza maisha, huku wengine watano wakijeruhiwa na kulazwa kwa ajili ya matibabu.

“Wakati wa tukio hilo, kundi hilo liliwashambulia askari na watu wengine waliokuwapo katika eneo hilo. Pia lilichoma moto gari aina ya Land Cruiser na kuchukua silaha moja ya kivita aina ya AK-47,” amesema Kamanda Lulengelule.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa lengo la kuwabaini wote waliohusika na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Lulengelule ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo vya dola katika kutatua migogoro inayojitokeza.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم