Ad
Breaking🔥

WAANDISHI WATAKIWA KUCHUNGUZA ATHARI ZA EL NINO

 WAANDISHI WATAKIWA KUCHUNGUZA ATHARI ZA EL NINO

Mwandishi Wetu | Arusha Digital – Dodoma

WAANDISHI wa habari za mazingira nchini wametakiwa kuacha kuishia kuripoti matamko ya viongozi kuhusu mvua za El Niño na badala yake kufanya uandishi wa uchunguzi utakaobaini mapema maeneo yenye hatari na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia madhara.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi kwa Jamii za Pembezoni (MAIPAC), Mussa Juma, wakati akifunga mafunzo ya waandishi wa habari za mazingira kutoka mikoa ya Kanda ya Kati yaliyofanyika Dodoma.


Mafunzo hayo yaliandaliwa na MAIPAC kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Juma alisema kutokana na utabiri wa uwezekano wa kunyesha mvua kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, waandishi wanapaswa kuanza sasa kuibua mapungufu yaliyopo katika maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

“Bado kuna mapungufu katika maeneo mbalimbali katika kukabiliana na athari za El Niño. Waandishi tusisubiri maafa yatokee, bali tuibue mambo yanayopaswa kufanywa sasa,” alisema.

Alisema baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara na miundombinu mingine inaendelea, lakini mifumo ya maji katika maeneo hayo haijawekewa mkazo wa kutosha, jambo ambalo linaweza kuongeza hatari ya maji kuelekezwa kwenye makazi ya wananchi wakati wa mvua kubwa.

“Tunapaswa kuandika sasa na kuhoji wakandarasi na wahusika kuboresha mifumo ya maji, badala ya kusubiri maafa yatokee ndipo tuanze kuandika,” alisema.

Juma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), aliwataka waandishi kutumia uandishi wa uchunguzi kufuatilia pia sababu za kuibuka kwa migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wahifadhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema migogoro hiyo imeendelea kusababisha madhara, ikiwamo vifo, hivyo waandishi wanapaswa kuchunguza chanzo cha migogoro hiyo, wahusika na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuzuia madhara zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi na Uendeshaji wa THRDC, Wakili Halima Sonda, aliwataka waandishi walioshiriki mafunzo hayo kutumia maarifa waliyopata kuboresha uandishi wao na kuleta tofauti katika namna wanavyoripoti masuala ya mazingira na haki za binadamu.

Sonda pia aliwakumbusha kuzingatia sheria na maadili ya uandishi wa habari wakati wa kutekeleza majukumu yao, akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na zenye kuzingatia maslahi ya jamii.

Mafunzo hayo yalishirikisha waandishi 35 kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya, Iringa na Singida.

Kwa mujibu wa waandaaji, mafunzo kama hayo tayari yamefanyika kwa waandishi kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Ziwa, huku programu nyingine zikitarajiwa kufanyika kwa waandishi kutoka Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Zanzibar.


Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post