Ad
Breaking🔥

ZARA YATWAA TENA TUZO YA UTALII AFRIKA

 ZARA YATWAA TENA TUZO YA UTALII AFRIKA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KAMPUNI ya utalii ya Zara Tanzania Adventures imeandika historia kwa kutwaa kwa mara ya pili mfululizo tuzo ya Africa’s Leading Adventure Tour Operator 2026, katika Tuzo za World Travel Awards – Africa, ikijidhihirisha kuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza katika sekta ya utalii wa adventure barani Afrika.

Zara ilitwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2025 na kurejea tena kileleni mwaka huu, hatua inayosisitiza nafasi yake katika kutoa huduma za utalii wa adventure zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Tuzo hiyo imetambua mchango wa kampuni hiyo katika kutoa huduma bora kwa watalii, kuendeleza utalii unaowajibika na kushirikisha jamii katika shughuli za utalii.

Kupitia shughuli zake, Zara huwaongoza watalii katika kupanda Mlima Kilimanjaro, ambao ni mrefu zaidi barani Afrika, pamoja na kuendesha safari za wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo mengine ya utalii nchini Tanzania.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa ushindi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Zara Tanzania Adventures, Zainab Ansell, amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa kampuni hiyo, wafanyakazi wake, washirika, wateja na jamii zinazoshiriki katika shughuli zao.

“Utambuzi huu mfululizo ni wakati wa fahari kwa timu ya Zara, washirika wetu, wateja wetu na jamii za karibu zinazofanya kila safari iwezekane. Kutoka Tanzania hadi Afrika nzima—Adventure Bila Kikomo,” amesema Ansell.

Amesema ushindi huo unaipa kampuni hiyo nguvu ya kuendelea kuboresha huduma na kuhakikisha wageni wanaopata fursa ya kutembelea Tanzania wanapata uzoefu wa kipekee.

Kwa mujibu wa Zara, ushindi huo wa mara mbili mfululizo unaonyesha pia nafasi ya Tanzania katika soko la utalii wa adventure duniani, hususan kupitia vivutio kama Mlima Kilimanjaro na Serengeti.

Mbali na huduma za kupanda Mlima Kilimanjaro na safari za wanyamapori, kampuni hiyo imeendelea kusisitiza utalii unaowajibika, uendelevu na ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za utalii.

Kutoka kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro hadi tambarare za Serengeti, Zara Tanzania Adventures imeendelea kushikilia taji la Africa’s Leading Adventure Tour Operator kwa mwaka wa pili mfululizo.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post